Kutoka Suez hadi Hormuz, Marekani haijajifunza kutokana na historia?
Chanzo cha picha, BBC/Getty images
Vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, sasa vimechukuwa mwenendo ambao hautabiriki.
Semi za Trump kupitia mtandao wake wa kijamii zimekuwa zikichochea vita hivyo na kuathiri masoko ya kimataifa.
Kando na semi za Trump historia pia ina mchango wake katika vita hivi.
Tangu kuanza kwa vita hivyo, wataalam wengi wamekuwa wakirejelea historia ili kuelewa kinachotokea na kitakachojirudia.
Matukio matatu ya kihistoria yanajitokeza katika suala hili.
Mfereji wa Suez
Chanzo cha picha, Hulton-Deutsch/Hulton-Deutsch Collection/Corbis via Getty Images
Baada ya kundi la wahouthi wa Yemen, kutekeleza mashambulizi dhidi ya Israel siku ya Ijumaa, ikiwa mashambulizi ya kwanza tangu kuanza kwa vita vya Israel na Marekani dhidi ya Iran, hatua hiyo imeanzisha vita vingine.
Kuingilia kati vita hivi na kundi hili ambalo ni mshirika wa karibu wa Iran, kunazua hofu ya kuhatarisha biashara ya dunia, kwani kundi hilo linauwezo wa kushambulia meli zinazopitia bahari ya shamu, haswa mfereji wa Suez.
Ingawa kundi hilo haliwezi kufunga kabisha mfereji huo wa bahari, ambao hupitisha 30% ya meli zote za bidhaa duniani, kundi hilo linaweza kuvuruga na kuzuia meli hizo kupitia eneo hilo. Pamoja na kuzuia kwa meli kupitia mlango bahari wa Hormuz wataalam wanasema hii itakuwa na athari kubwa sana kwa uchumi wa kimataifa.
Katika muktadha huu, wataalam wanaashiria mzozo wa mfereji wa Suez ulioshuhudiwa miaka 70 iliyopita.
Mwaka wa 1956, rais wa Misri Gamal Abdel Nasser alichukua udhibiti wa mfereji wa Suez, njia moja muhimu duniani ya usafirishaji mafuta. Ufaransa, Uingereza na Israel walijaribu kuichukua tena bila kufanikiwa.
Chanzo cha picha, Hulton-Deutsch Collection/CORBIS/Corbis via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa Trump na mshirika wake Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, historia inawapa mafunzo kadhaa.
"Zaidi ya yote, hili liliashiria mwisho wa Uingereza kuwa taifa lenye nguvu nyingi duniani," anasema Jeremy Bowen, mhariri wa masuala ya kimataifa wa BBC. "Uingereza ilikuwa ikitumia ushawishi wa kifalme katika Mashariki ya Kati tangu Vita vya Kwanza vya Dunia, na hili lilikuwa mwanzo wa mwisho wa ushawishi huo."
Mbinu za kivita zinazotumika sasa na Tehran za kuzuia usafiri kupitia mlango bahari wa Hormuz ni sawa na mbinu alizotumia Nasser.
Mwanahistoria wa Uingereza Alfred W.McCoy anasema kabla vikosi vya pamoja vya Uingereza na Ufaransa kufika katika mfereji wa Suez, tayari Nasser alikuwa ameshambulia na kuzamisha meli kadhaa na kufunga mfereji huo, na kusitisha usafirishaji wa bidhaa muhimu kuelekea ulaya na ghuba ya uajemi.
Rais wa Marekani wa kipindi hicho Dwight D. Eisdenhower, ambaye hakutaka kuingilia vita hivyo, kipindi cha vita baridi na muungano wa kisovyeti, aliingia kati na kuwalazimu Uingereza na Ufaransa kuachana na vita katika mfereji wa Suez.
"Wakati huo, Uingereza ilikuwa imewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa, uchumi wake ulikuwa karibu unaporomoka, uwezo wake wa kijeshi haukuwa imara na utawala wake wa kifalme ulionekana dhaifu" Aliandika McCoy.
Chanzo cha picha, Smith Collection/Gado/Getty Images
Mzozo wa mafuta mwaka wa 1973
"Mwaka wa 1973, vita vilizuka kati ya Israel, Misri, na Syria. Ilikuwa shambulio la ghafla dhidi ya Israel lililofanywa na Wamisri na Wasyria, vita vya Yom Kippur.
Marekani ilirusha mabomu Israel, anaelezea Bowen. "Kulipiza kisasi, mataifa ya Kiarabu yaliweka vikwazo ambavyo vilisababisha bei ya mafuta kupanda na kuathiri mataifa ya Ulaya"
Waziri wa mafuta wa Saudi wakati huo, Sheikh Ahmed Zaki Yamani, mwaka wa 1973 alionyesha jinsi rasilimali kama mafuta, inaweza kutumika kama chombo cha ushawishi na kuathiri uchumi wa dunia.
Alielezea kuwa nguvu kubwa ya mataifa ya kiarabu ni "silaha ya mafuta" inayoweza kuchochea kuanguka kwa uchumi wa dunia.
Vikwazo hivyo vilidumu kwa miezi mitano, lakini wataalamu wanaamini madhara yake yalidumu kwa kipindi cha muongo mmoja.
Chanzo cha picha, Hulton Archive/Getty Images
Ingawa mafuta ghafi, hayana tena umaarufu mkubwa kimataifa kama ilivyokuwa miaka 50 iliyopita, mahitaji yake yakiwa yamepungua, bado ni rasilimali muhimu katika mataifa ya magharibi.
Ingawa Marekani sasa inazalisha nishati zaidi kuliko inavyotumia tofauti na nusu karne iliyopita, bado taifa hilo linaagiza kiasi kikubwa cha mafuta ghafi na huenda bei ya mafuta ikapanda nchini humo na kuwaathiri raia wa taifa hilo.
Marekani pia inaweza kuathiriwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja na changamoto zinazoikabili washirika wake wakuu wa kibiashara bara Asia, ambao wanategemea pakubwa mafuta kutoka mataifa ya Ghuba na sasa wameanza kushuhudia upungufu wa bidhaa hiyo.
"Kinachoendelea sasa hivi taifa la Saudi, Falme za Kiarabu, na mataifa mengine hawajatoa taarifa ya kutouiuzia Ulaya mafuta, lakini Iran na Wahouthi inafanya iwe vigumu sana wao kufikia masoko ya kimataifa na kusafirisha mafuta hayo"anaelezea Bowen.
Vita vya Iraq na Iran
Wanahistoria wanasema vita vya Iraq na Iran miaka ya 1980, zinampa Trump viashiria tosha jinsi mashambulizi ya Marekani yaanathiri njia muhimu za ushafirishaji bidhaa na soko la dunia.
Katika mwisho wa vita hivyo mlango bahari wa Hormuz, ulilengwa na Tehran na Baghdad, kama njia moja ya kuwashirikisha mataifa yenye nguvu katika vita hivyo.
Katikati mwa miaka ya 1980, vita hivyo vilitanuka zaidi hadi Kuwait ikaitisha msaada wa kimataifa ili meli zao ziweze kupitia mlango wa Hormuz. Washinton ilikubali kuisaidia Kuwait, ili kuikomoa Urusi, adui wao katika vita baridi wakati huo.
Chanzo cha picha, Barry Iverson/Getty Images
Oparesheni hiyo iliyoitwa Earnest Will,the tanker escort, ilianzishwa mwaka wa 1987, ila haikufanikiwa baada ya meli ya Kuwait iliyofaa kulindwa na Marekani, ililengwa na mabomu ya majini ya Iran, ikielekea Kuwait.
Tukio hilo kulingana na wataalam lilionyesha udhaifu wa Marekani kukosa kuondoa mabomu ya majini katika mlango huo wa bahari, suala ambalo liliathiri pakubwa oparesheni hiyo.
Katika vita vya sasa, Trump ametoa wito kwa mataifa mengine kuingilia kati kufungua mlango bahari wa Hormuz na kutoa ulinzi kwa meli zinazopita eneo hilo.
Ila wataalam wanasema Washington inakumbwa na changamoto kubwa kwa sasa, kwani silaha za vita zimeboreshwa zaidi na sasa kuna matumizi ya ndege zisizo na rubani, na Iran na Iraq si maadui tena.
Habari kuu
Gumzo mitandaoni
Zinazovuma zaidi
Haipatikani tena