WARIDI WA BBC: 'Namlea mwanangu anayenitegemea saa 24 bila kupumzika'
Chanzo cha picha, Loice Mwende
Katika mazingira tulivu, eneo la Githurai, jijini Nairobi, tunakutana na Loice Mwende, mlezi wa kijana wake aliyempa jina la Kariuki mwenye umri wa miaka minne ambaye ana tatizo la Cerebral Palsy, yaani utindio wa ubongo.
Mama huyu mwenye azma ya dhati amejitolea maisha yake kumlea mwanawe wa pekee huku akijitahidi kupenya katika ulimwengu ambao mara chache hutoa fursa kwa ajili yake na hali ngumu ya kifedha na uchovu wa kihisia vikitishia kumlemea.
Mwezi mzima wa Machi unatambulika kuwa wa kitaifa katika uhamasishaji wa tatizo la kupooza kwa ubongo.
Asha Juma alimtembelea mama huyo na kutuandalia makala ifuatayo inayozungukwa na uvumilivu, kujitolea na upendo usio na kipimo wenye kuonyesha nini maana ya kumpigania mwingine bila masharti wala ukomo.
Safari ya maisha
Loice Mwende akianza kutafakari safari yake ya ujauzito ilivyokuwa, anasema hali haikuwa rahisi. Mume wake aliugua na kulazwa hospitalini kwa muda. Na kwa sababu hakuwa anafanya kazi, ilifika kipindi akafungiwa nyumba kwa kukosa kodi na ikabidi aishi kama mtoto wa mtaani.
"Mume wangu alipolazwa, sikuwa na mahali pa kuishi na nikalazimika kuwa kama mtoto wa mitaani. Marafiki walinikataa, nyumbani nilikifukuzwa, sikuwa na pakwenda," Loice anasema.
Akiwa anafikiria kuwa kuwa mume wake alimuacha, kumbe alikuwa hospitalini kipindi cha miezi sita, hajui aingiae wala atokaye.
Mumewe alikuwa amekosa fahamu kabisa na wakati ambapo amekata tamaa, alisikia simu yake asijue kwamba ni baba mtoto anayemtafu.
Baada ya kupoteleana kwa muda, wakaunganishwa tena na manani na kuendela na maisha kama kawaida. Loice hakujua kumbe ilikuwa furaha ya muda tu.
'Mtoto wangu alianza kuwa mweupe kuzeeka kabisa'
Chanzo cha picha, Loice Mwende
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati wa kujifungua ulipowadia. Loice alikwenda hospitali kupata mtoto akijua kuwa kila kitu kitakwenda sawa.
"Chupa ya mtoto ilipasuka na maji yakaanza kumwagika. Mimi sikuwa na uchungu kama wengine. Lakini nilizunguka hospitali kadhaa kabla ya kupata ile ambayo ilinikubali kunizalisha," Loice anakumbuka.
Wakati akidhani amepata afueni, Loice alikumbana na siku tatu za majaribu zilizofuata na kuongeza kuwa baada ya kijifungua alizimia.
"Nilikuwa nikiambiwa zunguka zunguka kila siku hadi ikafika siku ya nne. Nilipojifungua nilisikia mtoto akilia, na baada ya hapo nikapoteza fahamu kwa saa mbili", Loice anasema.
"Nilipata uchungu wa kujifungua kwa muda mrefu, nilimwaga maji siku nne bila kushughulikiwa, ya tano nikapata mtoto ambaye alipelekwa chumba cha kufuatilia watoto wakiwa katika hatari. Akalazwa wiki mbili," Loice anaelezea.
Lakini kama haitoshi, alianza tukio ambalo hakuwa amewahi kulishuhudia maishani mwake.
"Kesho yake mtoto wangu alikuwa mweupe na akazeeka kabisa. Hapo ndio alipelekwa kwenye chumba cha walio katika hatari ili kupata matibabu," Loice anasema.
Lakini licha ya hali hiyo Loice anasema daktari hakumueleza chochote kuhusu hali ya mtoto wake.
Kukubaliana na ukweli mchungu
Chanzo cha picha, Loice Mwende
Mtoto akiwa na miezi kumi na moja hapo ndipo Loice alianza kuwa na wasiwasi juu ya hali ya mwanawe.
"Kuna rafiki yangu ambaye tulipishana kubeba ujauziot kwa mwezi mmoja, akawa ananiuliza, mtoto wako anafanya hivi na hivi nikawa namjibu hapana, hapo ndipo nilipokata ushauri wa kwenda kumuona daktari," Loice anasema.
"Daktari tuliyekwenda kumuona, hakutuambia moja kwa moja kuwa mtoto anatatizo. Yeye alisema misuli ya mtoto imekazana na tutaitaji mtaalamu wa viungo kwa miezi miwili."
Bado Loice akiwa hajapata jibu sahihi ya kile ambacho mtoto wake anapitia, jirani yake alikuwa na mtoto kama wake na yeye ndiye aliyekuja kumtoa taka za machoni.
"Huyu mama alinichukua akanipeleka hospitali ambayo alikuwa akipeleka mtoto wake."
Na daktari wake ndiye aliyemwambia ukweli kuwa mtoto wake amepata tatizo la utindio wa ubongo.
Haikuwa rahisi kwa Loice kukubali hali halisi ya mtoto wake kwa sababu alikuwa na ufahamu mdogo kuhusu tatizo hili, na pia aliamini linaweza kutokea kwa yule ambaye amekuwa akitatiza wengine katika jamii.
"Mimi niliamini kwamba ili kupata tatizo kama hili, lazime uwe ulikuwa mtu mbaya, na kila nikijiangalia na kufikiria nilipotoka, niliamini hakuna niliyemkosea, au aliye ni laani ili nipate mtoto mwenye utindio wa ubongo," Loice anasema.
Moja ya changamoto kubwa kwa Loice alizokumbana nazo ni kukubali hali ya mtoto wake.
"Babu yake mtoto alikuja akanikuta ninataka kumuua. Nilikuwa nimemshika miguu nikitaka kumgonga kitandani. Nilikuwa mpaka na dawa na kisu. Nilichopanga ni kuwa nikimaliza kumuua na mimi nijiue," Loice alisema.
Hapa ndio familia ya mume wake iligundua kuwa mama Kariuki ana matatizo ya afya ya akili na kulazimika kutafuta matibabu.
"Nilipelekwa hospitali ya wagonjwa wa akili na kuanza kupata tiba," Loice anasema.
Na baada ya matibabu, alirejea nyumbani akiwa mwingi wa majuto kila alipofikiria kile alichokuwa anataka kumfanyia mtoto.
Mambo yalivyobadilika
Safari ya kupona kwa Loice ikaanza hatua kwa hatua na taratibu akapata moyo wa chuma. Anasema mambo yalianza kufunguka yenyewe.
Lakini ni namna gani Loice alipata msukumo wa kusonga mbele?
"Kariuki tu, ni mtoto wangu, nampenda yaani kitu chochote ninachofanya katika haya maisha yangu, kiwe kibaya au kizuri ni sababu yake tu," Loice anasema.
"Huyu mtoto ananitegemea saa 24 bila kupumzika, kuanzia asubuhi mpaka usiku ni mimi na huyu mtoto."
"Mungu akitupatia Kariuki, siyo kuwa hakuwa anajua anachofanya. Sasa, kile tutakachofanya, hata changamoto zije, tuko pamoja na huyu mtoto. Mimi na mtoto wangu nitasimama na yeye vizuri. Nitamlea, hata kama nikulala njaa. Hata kama atakosa nepi, ni sawa tutakaa hivyo, lakini ni mimi na Kariuki hadi mwisho," Loice anasema.
Safari ya matibabu ya Kariuki japo imekuwa na changamoto si haba, mama yake anamshukuru Mungu kwa sababu, kila akitizama alikotoka ana kila sababu ya kutabasamu.
"Kwa sasa hivi tunavyozungumza, mtoto wangu shingo yake imeanza kujitegemea, uti wa mgongo umerudi vizuri. Ulikuwa umepinda, ulikuwa nje. Sasa hivi, mtoto wangu anaweza kurusha rusha miguu yake. Hali ya mtoto wangu imeimarika. Anaweza akaniita mama," Loice anasema.
"Kama mama yake mtoto, nitalia na yeye na kufurahi na yeye"
Loice anasema kile anachoweza kushauri kina mama wengine wanaopitia changamoto kama yeye, kwanza ni kujikubali ndio upate nguvu ya kusonga mbele.
Hata kuwe na changamoto gani inabidi uwe wa kwanza kujituma na kuonyesha kwanini wengine wajitokeze kukusaidia.
Ushauri na daktari
Keith Kaime daktari wa viungo vya mwili, anaelezea ni muda gani sahihi wa kuanza kupata matibabu kama haya.
"Muda muafaka wa kuanza matibabu kwa mtoto kama Kariuki ni kuanzia siku ya kuzaliwa. Huwa tunasema, kuanza mapema, ndio maamuzi bora zaidi. Kwa hivyo, mzazi hafai kuchelewa."
"Ukichelewa, mtoto atarudi nyuma. Ule muda ambao alikuwa anafaa kuchukua kutimiza hatua fulani za kukua. Ukichelewa atachelewa, ukianza mapema atashika mapema".
Daktari Kaime anasema matibabu ya aina hii hayana mwisho lakini inategemea mwitikio wa mtoto kwa matibabu na kuongeza kuwa moja ya changamoto pia ni pale unapojitahidi kutoa matibabu lakini unaona inachukua muda kuona matokeo, ingawa anasema hili linategemea na ubongo wa mtoto na uvumilivu.
Hakika haijakuwa rahisi kwa mama Kariuki ambaye pia anawakilisha kina mama wengi wanaopitia changamoto za aina hii, lakini hatua zozote hata kama ni kidogo kiasi gani, kuanza kutamka, kucheza utagundua kuwa siyo tu kufanya kitu kwa usahihi bali ni kufanya na kufanya tena.
Wakati unapokumbana na kitu ambacho hukukitarajia kama tatizo hilo, itakuwa muhimu ikiwa utakabiliana na hofu yako na kumkubalia mwanao kukabiliana na dunia.
Habari kuu
Gumzo mitandaoni
Zinazovuma zaidi
Haipatikani tena