Waridi wa BBC: Muundaji maudhui aelezea safari ngumu aliyopitia katika kupunguza uzito

Chanzo cha picha, Lydia Wanjiru

Maelezo ya picha, Lydia Wanjiru
    • Author, Phyllis Mwatee
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Lydia Wanjiru amefunguka kuhusu safari yake ya mabadiliko ya mwili, akieleza jinsi alivyopunguza uzito kwa kiasi kikubwa kabla ya kuamua kufanyiwa upasuaji wa urembo, kupunguza mafuta kwenye tumbo lake na kuongeza makalio yake.

Anasema alianza kwa kupunguza uzito kwa kupoteza kilo 34, akishuka kutoka kilo 104. Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, anasema alibaki na changamoto ya ngozi iliyolegea sana, hali iliyomfanya kutoridhika na muonekano wake.

Lydia anasema, mazoezi pekee hayakutosha kurekebisha hali hiyo. Alieleza kuwa kupunguza uzito ni mchakato unaohitaji nidhamu ya lishe na mazoezi.

Hatahivyo harakati zake za kutafuta tiba ya haraka ilifanikiwa baada ya kupata dawa kwa jina GLP-1 kwa miezi minane iliyochangia mafanikio yake ya kupungua uzito.

Chanzo cha picha, Lydia Wanjiru

Maelezo ya picha, Lydia Wanjiru

Ngozi inayoning'inia

Baada ya hapo, alianza kutafuta suluhisho la kudumu kwa ngozi yake iliokuwa ikining'inia. Alifanya mashauriano mbalimbali kabla ya kufikia uamuzi wa kufanyiwa upasuaji.

Daktari aliyemhudumia alimweleza kuwa licha ya kupunguza uzito, hakuwa na misuli ya kutosha kusaidia mwili kuwa katika umbo linalotakiwa.

Hatimaye, Lydia alifanyiwa upasuaji wa kuondoa ngozi tumboni, ambapo takribani kilo mbili za ngozi ziliondolewa.

Pia alifanya taratibu nyingine za urembo ikiwemo kufyonza mafuta yaliyozidi mwilini kwa kutumia bomba dogo {liposuction,} na upasuaji wa kuondoa ngozi iliyolegea na mafuta mengi, pamoja na kushona misuli ya tumbo iliyolegea {tummy tuck na BBL.}

Gharama ya matibabu hayo ilifikia takribani milioni 1.5 pesa za Kenya ikiwa ni sawa na USD 11,600 ingawa anasema kiasi hicho hutegemea mahitaji ya mtu binafsi.

Tazama hapa
Maelezo ya video, Waridi wa BBC: Muundaji maudhui aelezea safari ngumu aliyopitia katika kupunguza uzito

Je, safari yake ya kupona ilikuwaje?

Anasema kuwa safari ya kupona haikuwa rahisi. Alilazimika kukaa hospitalini kwa siku kadhaa na alipata maumivu makali, hasa siku za mwanzo baada ya upasuaji.

Katika kipindi hicho, alihitaji msaada wa karibu kwa shughuli za kawaida za kila siku.

Alikuwa akisaidiwa kuoshwa hata baada ya kwenda haja.

Baada ya kutoka hospitalini, aliendelea na matibabu ya kusaidia mwili kupona, ikiwemo "masaji ya kutoa majimaji mwilini" au "tiba ya kanda ya mfumo wa limfu" {lymphatic massage} ya kila siku.

Anakiri kuwa kulikuwa na nyakati za kujuta kutokana na maumivu, lakini hali ilibadilika kadri muda ulivyopita na mwili kuanza kuimarika.

Licha ya changamoto hizo, Lydia anasema ameridhika na matokeo na anaamini uamuzi wake ulimsaidia kuongeza kujiamini. Anaongeza kuwa atafanya tena upasuaji huo akipata nafasi.

Chanzo cha picha, Lydia Wanjiru

Maelezo ya picha, Lydia Wanjiru

Kufanya maamuzi magumu

Hata hivyo, anasisitiza kuwa jambo muhimu zaidi ni mtu kujipenda kabla ya kufanya uamuzi wowote wa kubadilisha mwili. Anatahadharisha dhidi ya kufuata mitindo ya mitandao ya kijamii bila kufanya utafiti wa kina au kushauriana na wataalamu.

Kuhusu suala la uzazi, Lydia amesema amechagua kutopata watoto, na kwamba uamuzi huo pia uliathiri maamuzi yake kuhusu mabadiliko ya mwili wake.

Lydia anasema kwamba kila mtu ana safari yake ya kipekee, na maamuzi kuhusu mwili yanapaswa kufanywa kwa uelewa, si kwa shinikizo la jamii au kulinganisha maisha na wengine.