Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yasema ina 'karata mpya' vita vikirejea, mazungumzo yakiwa shakani

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo bado kuna sintofahamu kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo mapya ya kumaliza vita kati ya pande hizo mbili huko Pakistan.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Trump ni 'muongo' - Iran

    Shirika la habari la Fars lenye mafungamano na kikosi cha walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) limechapisha nukuu kwenye mtandao wa Telegram kutoka kwa kamanda katika makao makuu ya kijeshi ya Iran. Nukuu inayomkosoa Rais wa Marekani, Donald Trump, kwamba amekuwa akisema uongo.

    Akiandika kwa Kiajemi, Meja Jenerali Abdullahi anasema kwamba IRGC imefanikiwa kuisukuma Israel na Marekani hadi kufikia hali ya kukata tamaa na uchovu,na kuwalazimu kuomba kwa dharura kusitishwa mapigano, kwa mujibu wa Fars.

    Anasema vikosi vya kijeshi visingemruhusu "rais wa Marekani muongo na mdanganyifu" "kutunga maelezo ya uongo kuhusu hali ilivyo katika uwanja wa vita haswa kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz.

    Bado haijulikani wazi ikiwa ujumbe wa Iran utaelekea Islamabad kwa duru ya pili ya mazungumzo ya amani na Marekani.

    Trump hakupatanikana mara moja kuelekeza hilo, lakini mara kadhaa amekanusha kuhusu tuhuma za kudanganya, akisimamia msimamo wa Marekani kwenye mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

    BC Asia Kusini anaeleza, kuna mvutano wa kisiasa nyuma ya pazia nchini Iran, huku watu wenye msimamo mkali wakiweka shinikizo kwa wapatanishi kuchagua mzozo badala ya diplomasia.

    Unaweza kusoma pia:

  2. Pakistan iko kwenye nafasi ya kipekee kuandaa mazungumzo, huku ikikabiliwa na hatari

    Pakistan iko katika nafasi ya kipekee ya kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani, lakini hatua hiyo inaambatana na hatari kubwa kwa nchi hiyo.

    Wakati Pakistan ikijiandaa kwa duru ya pili ya mazungumzo hayo ingawa bado kuna mashaka ikiwa yatafanyika usalama unaimarishwa sana mjini Islamabad.

    Aidha, mabango yenye ujumbe wa “Mazungumzo ya Islamabad” yanaonekana kote katika mitaa ya mji mkuu huo.

    Nchi hiyo ina nafasi maalum kwa sababu inaaminika na mataifa mbalimbali yenye ushawishi mkubwa kama Marekani, Iran na nchi za Ghuba.

    Hali hii inaifanya Pakistan kuwa kiunganishi muhimu katika juhudi za kidiplomasia zinazolenga kupunguza mvutano katika eneo hilo lenye migogoro ya mara kwa mara.

    Hata hivyo, uhusiano wa karibu wa Pakistan na Marekani haukuizuia kulaani rasmi mashambulizi ya awali ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Ikiwa mazungumzo yatavunjika, Pakistan inaweza kujikuta ikipigana na jirani yake Iran.

    Pakistan ilisaini mkataba wa ulinzi wa pande zote na Saudi Arabia mwaka jana, moja ya nchi za Ghuba ambazo zimeathiriwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Iran kabla ya usitishaji mapigano wa sasa, ambao unatarajiwa kuisha kesho.

  3. Safari za meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz zinapaswa kuendelea - Xi Jinping

    Rais wa China Xi Jinping anasema "safari za kawaida za meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz "zinapaswa kuendelea".

    Alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman siku ya Jumatatu.

    Xi alisema kuwa njia hiyo muhimu ya baharini inapaswa kubaki wazi kwa matumizi ya kawaida, kwa sababu ni kwa manufaa ya nchi za eneo hilo pamoja na jamii ya kimataifa kwa ujumla.

    Kwa upande mwingine rais wa Marekani Donald Trump na Xi wanatarajiwa kukutana nchini China mwezi Mei, baada ya safari hiyo kuahirishwa awali kutokana na vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Unaweza kusoma pia:

  4. Iran yasema ina 'karata mpya' vita vikirejea, mazungumzo yakiwa shakani

    Kadiri muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani, Israel na Iran unavyokaribia kuisha, bado hakuna uthibitisho wa mazungumzo zaidi ya amani.

    Spika wa bunge la Iran aliandika kwenye mtandao wa X akisema kwamba Iran imekuwa "ikiandaa mkakati mpya kwa ajili ya uwanja wa vita" katika wiki mbili zilizopita na "haitakubali mazungumzo chini ya kivuli cha vitisho".

    Wakati huo huo, Rais Donald Trump amekanusha kwamba yuko chini ya shinikizo la kufanya makubaliano, huku vyombo vya habari vya Marekani vikiripoti kwamba makamu wa rais JD Vance atasafiri kwenda Pakistan Jumanne kwa mazungumzo.

    Katika Ghuba, Marekani inaendelea kuzuia Mlango wa Hormuz baada ya kukamata meli ya mizigo yenye bendera ya Iran siku ya Jumapili na pande zote mbili zinashutumiana kwa ukiukaji wa mapigano.

    Kwingineko, duru ya pili ya mazungumzo kati ya Israeli na Lebanon inatarajiwa kufanyika Alhamisi kwa mujibu wa afisa wa Marekani.

  5. Wachimbaji haramu 42 wanaswa Nigeria baada ya kiongozi wa jadi kutekwa

    Polisi katika jimbo la Kwara nchini Nigeria wamewakamata washukiwa 42 wa uchimbaji haramu kufuatia kutekwa nyara kwa kiongozi wa jadi, huku hofu ya usalama ikizidi kuongezeka katika eneo hilo.

    Mfalme Oba Salman Olatunji Aweda, wa jamii ya Olayinka katika eneo la serikali ya mtaa ya Ifelodun, alitekwa nyara Jumamosi jioni baada ya watu wenye silaha kuvamia ikulu yake.

    Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu, kamishna wa Polisi wa Jimbo la Kwara, Adekimi Ojo, alisema kukamatwa kwao ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu utekaji nyara huo.

    Hata hivyo, alisisitiza kwamba haijabainika ikiwa walihusika moja kwa moja katika shambulio hilo.

    Kwa mujibu wa polisi, takriban wanaume kumi wenye silaha nzito walivamia ikulu muda mfupi baada ya wachimbaji wanaofanya kazi katika eneo hilo kumtembelea mfalme mapema siku hiyo.

    Washambuliaji hao wanaripotiwa kudai pesa kwa kiongozi huyo wa kitamaduni kabla ya kumtoa chumbani kwake.

    Bw. Ojo alisema mfalme alikabidhi pesa hizo lakini bado alichukuliwa pamoja na kaka yake.

  6. Raia wa Canada auawa kwa risasi katika eneo la kale nchini Mexico

    Mwanamke mmoja raia wa Canada ameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baada ya mtu aliyejihami kwa silaha kufyatua risasi katika eneo la kihistoria nchini Mexico, kwa mujibu wa maafisa wa nchi hiyo.

    Tukio hilo limeibua hofu na maswali kuhusu usalama katika maeneo maarufu ya utalii. Shambulio hilo lilitokea katika eneo la kumbukumbu ya kale la Teotihuacán lililopo kaskazini mwa Mexico City siku ya Jumatatu.

    Serikali ya Mexico ilisema mshambuliaji huyo alijiua baada ya kutekeleza tukio hilo.

    Polisi walipofika eneo la tukio walikuta bunduki, silaha yenye makali pamoja na risasi ambazo hazikutumika.

    Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum alisema "Kilichotokea leo huko Teotihuacán kinatuumiza sana. Ninatuma salamu za pole na rambirambi kwa waathiriwa na familia zao," aliandika kwa Kihispania.

    Piramidi na magofu ya kale ya Teotihuacán ni eneo la urithi wa dunia lililotambuliwa na UNESCO, ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya watalii nchini Mexico.

    Tukio hilo linaweza kuathiri taswira ya usalama katika maeneo hayo muhimu ya kihistoria.

    Waziri wa mambo ya nje wa Canada Anita Anand alithibitisha kuwa raia mmoja wa Canada aliuawa na mwingine kujeruhiwa

  7. Tahadhari ya ujio wa tetemeko yatangazwa Japan baada ya kuondoa onyo la Tsunami

    Maafisa nchini Japani wameonya kuhusu tetemeko la ardhi "kubwa" linalotarajiwa katika wiki ijayo baada ya tetemeko la ukubwa wa richa 7.7 kutokea pwani ya kaskazini-mashariki, na kusababisha amri ya kuhama na maonyo ya mawimbi ya tsunami ya mita 3 (futi 10).

    Maelfu ya watu waliamuriwa kuondoka katika maeneo ya pwani kwenda kwenye maeneo ya juu baada ya tetemeko hilo katika karibu na mkoa wa Iwate, kilomita 530 (maili 330) kaskazini mwa mji mkuu Tokyo.

    Mawimbi makubwa zaidi ya tsunami yalikuwa na urefu wa sentimita 80. Onyo la ujio wa Tsunami liliondolewa saa chache baada ya tetemeko hilo Jumatatu.

    Lakini shirika la hali ya hewa la Japan limeonya kwamba matetemeko "yanayosababisha tetemeko kubwa zaidi" yanaweza kutokea katika wiki ijayo, na kusababisha mawimbi makubwa zaidi.

    Mamlaka ilisema kuna uwezekano wa kutokea tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa richa 8.0 au zaidi kuliko wakati wa kawaida.

    Japan ina kumbukumbu za tetemeko kubwa la ardhi lililotokea mwaka 2011 lililosababisha tsunami iliyogharimu maisha ya zaidi ya watu 18,000 na kusababisha kuyeyuka kwa kinu cha nyuklia cha Fukushima.

  8. Marekani haitaondoa kizuizi cha kijeshi Hormuz hadi makubaliano na Iran yafikiwe - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa nchi yake haitaondoa kizuizi ilichoweka kwenye bandari za Iran hadi pale makubaliano rasmi yatakapofikiwa na Tehran.

    Kauli hiyo imekuja wakati ambapo bado kuna sintofahamu kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo mapya ya kumaliza vita kati ya pande hizo mbili.

    Kizuizi hicho, ambacho kilianza wiki moja iliyopita, "kinaiangamiza Iran kabisa", Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii wa Truth Social, akiongeza kuwa nchi yake ilikuwa ikishinda mzozo huo "kwa kiasi kikubwa".

    Maoni yake yanaambatana na makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran yanayotarajiwa kukamilika Jumatano, lakini bado hakuna uhakika ikiwa awamu ya pili ya mazungumzo ya amani itaendelea nchini Pakistan.

    Usalama umeimarishwa katika mji mkuu wa Pakistan kufuatia mkutano huo. Hata hivyo makamu wa rais wa Marekani JD Vance anayetarajiwa kuongoza ujumbe wa Marekani bado hajaondoka Washington, huku Iran ikisema bado haijaamua kuhudhuria.

  9. Karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Aprili 21, 2026