Rais wa Taiwan afuta safari yake baada ya nchi za Afrika kufunga anga
Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, amefuta ziara yake katika taifa la Eswatini, akidai kuwa Beijing imeweka shinikizo kwa mataifa jirani ili kuzuia ndege yake kupita katika anga lao.
Nchi za Seychelles, Mauritius na Madagascar zilifuta vibali vya anga kwa ndege ya Lai baada ya “shinikizo kubwa” na mbinu za kiuchumi kutoka China, kwa mujibu wa afisa wa Taiwan.
China ilikanusha kutumia shinikizo hilo, huku ikiyasifu mataifa hayo matatu na kusema ina “thamani kubwa” kwao.
Hii ni mara ya kwanza kufahamika hadharani ambapo kiongozi wa Taiwan amelazimika kufuta safari ya nje kutokana na kufutwa kwa vibali vya kupita anga za nchi nyingine.
Eswatini, iliyojulikana zamani kama Swaziland, ndiyo mshirika pekee wa kidiplomasia wa Taiwan barani Afrika.
Ni moja ya nchi 12 pekee nyingi zikiwa ndogo katika Amerika ya Kusini au Pasifiki zinazoitambua Taiwan.