Mataifa ya Afrika Mashariki kuanzisha mradi wa pamoja wa kiwanda cha mafuta
Nchi za Afrika Mashariki zinaendelea kujadili mpango wa kujenga kiwanda cha pamoja cha kusafishia mafuta katika bandari ya Tanga, Tanzania, kwa mfano wa kiwanda cha Dangote cha Nigeria, amesema rais wa Kenya William Ruto siku ya Alhamisi.
Kwa sasa, Afrika Mashariki huagiza mafuta yote yaliyosafishwa, hasa kutoka Mashariki ya Kati, hali inayofanya eneo hilo kuwa katika hatari ya kupanda kwa bei na usumbufu wa upatikanaji wa mafuta, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mzozo wa Iran.
“Tutakuwa na kiwanda cha pamoja cha kusafishia mafuta Tanga ambacho kitawanufaisha wote, kwani kitachakata mafuta kutoka Jamhuri ya demokrasia ya Congo, Kenya, Sudan Kusini na Uganda,” alisema Ruto katika mkutano wa ufadhili wa miundombinu uliofanyika Nairobi.
Mfanyabishara tajiri zaidi barani Afrika, Aliko Dangote, ambaye pia alihudhuria mkutano huo, alisema anaweza kuanzisha mradi Afrika Mashariki kama wa kiwanda chake cha Nigeria kinachozalisha mapipa 650,000 ya mafuta kwa siku, endapo serikali za eneo hilo zitaunga mkono mpango huo.
Unaweza kusoma pia:Aliko Dangote aongoza orodha ya watu matajiri zaidi Afrika 2026