Hatujaomba kusitisha vita na hatuoni sababu - Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema nchi hiyo ‘haijawahi kuomba kusitishwa kwa vita’ katika vita vinavyoendelea kaati yake na nchi za Israel na Marekani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Iran: Hatujaomba mazungumzo ya kusitisha vita

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Iran “haijawahi kuomba kusitishwa kwa vita, wala hata kuomba mazungumzo na Marekani.”

    Kauli hiyo inafuatia kauli ya awali ya Donald Trump aliyedai kuwa Iran ilitaka kufanya mazungumzo, lakini yeye hakuwa tayari kuyakubali kwa sababu masharti yake hayatekelezeki.

    “Hatuoni sababu yoyote ya kuzungumza na Wamarekani, kwa sababu tulikuwa tayari tunazungumza nao wakati wao waliamua kutushambulia,” ameiambia CBS News.

    Ameongeza kusema: “Hii ni vita vilivyochaguliwa na Rais Trump pamoja na Marekani, na sisi tutaendelea kujilinda.”

  2. Iran yafungua mlango wa mazungumzo kuhusu Hormuz

    xcv

    Chanzo cha picha, Royal Thain Navy

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema nchi hiyo ‘haijawahi kuomba kusitishwa kwa vita’ katika vita vinavyoendelea kati yake na nchi za Israel na Marekani.

    Abbas Araghchi, ameiambia CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, kuwa Iran ipo wazi kwa mazungumzo na nchi yoyote inayotaka kuhakikisha usafirishaji wa meli kupitia mlango wa bahari ya Hormuz unafanyika kwa usalama.

    Eneo hili limekuwa likikumbwa na mashambulizi ya Iran dhidi ya meli, ambayo yamesababisha kusimama kwa shughuli za usafirishaji.

    Bila kutaja nchi maalum, Araghchi amesema kuwa idadi kadhaa ya nchi tayari zimeonyesha nia ya kushirikiana na Iran ili kulinda usalama wa usafirishaji katika eneo hilo.

    Aidha, amefafanua kuwa vifaa vyote vya nyuklia vya Iran viko chini ya uangalizi mkali wa kimataifa, na kwa sasa "hakuna mpango wowote wa kuvikarabati".

    Araghchi ameeleza kuwa wakati mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu mkataba wa nyuklia yalipokuwa yanaendelea, Iran ilitoa pendekezo la kupunguza kiwango cha nyenzo za nyuklia zilizokuwa zimeimarishwa hadi kiwango cha chini.

    "Hii ilikuwa punguzo kubwa," amesema. Hata hivyo, mzozo wa kisiasa umebadilisha hali hii: "Hakuna lolote mezani kwa sasa, kila kitu kinategemea mustakabali wake."

    Pia unaweza kusoma:

  3. Zelensky aishutumu EU kwa kuishinikiza Kyiv kufungua bomba la mafuta ya Urusi

    xcv

    Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameshutumu Umoja wa Ulaya kwa kujaribu "kushinikiza" Kyiv ili ifungue tena bomba la mafuta linalosafirisha mafuta ya Urusi kwenda Hungary na Slovakia.

    Alisema kurejesha uingizaji wa mafuta ya asili ya Urusi kupitia Ukraine kuelekea Umoja wa Ulaya (EU) nis awa na kuondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Moscow.

    Ukraine inasema bomba la mafuta la enzi ya Sovieti la Druzhba liliathiriwa na mashambulizi ya anga ya Urusi mwezi Januari na bado halijarekebishwa.

    Hungary inategemea mafuta ya Urusi na inazuia vikwazo vipya vya EU dhidi ya Moscow pamoja na mkopo muhimu wa €90 bilioni ($103 bilioni; £78 bilioni) kwa Kyiv hadi bomba hilo lifunguliwe.

    Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban, amekuwa na mvutano na Ukraine kuhusu suala hilo kuu kabla ya uchaguzi wa Aprili.

    Chama chake kipo nyuma katika kura za maoni.

    EU imemuhimiza Zelensky kurekebisha bomba hilo haraka na kumtaka kuruhusu wakaguzi.

    Baadhi ya maafisa wa EU wanahofia upinzani wa Zelensky unaweza kumsaidia Orban kushinda tena.

    Lakini akizungumza na waandishi wa habari mjini Kyiv, wakiwemo wa BBC, Zelensky alisema kuwa , anapinga mafuta ya Urusi kusafirishwa kupitia Ukraine huku EU ikipiga marufuku uuzaji wake sehemu nyingine.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Bobi Wine aondoka Uganda kwa muda baada ya kujificha kwa miezi miwili

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema ameondoka nchini humo kwa muda baada ya kujificha kwa takribani miezi miwili.

    Katika video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Bobi Wine alisema anasafiri kwenda nje ya nchi kwa kile alichokiita mikutano muhimu, ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu safari hiyo.

    Mwanasiasa huyo, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alionekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya wiki kadhaa kupitia video ya dakika tano iliyochapishwa kwenye mtandao wa X.

    Bobi Wine alisema alilazimika kukimbia nyumbani kwake mjini Kampala baada ya vikosi vya usalama kuvamia makazi yake kufuatia uchaguzi wa Januari, ambao anadai ulijaa udanganyifu na upendeleo kwa rais wa muda mrefu, Yoweri Museveni.

    Mwanamuziki huyo wa zamani aliyegeuka kuwa mwanasiasa alisema alifanikiwa kukwepa kukamatwa na sasa ameondoka nchini, lakini ameahidi kurejea kuendelea na mapambano yake ya kisiasa.

    Hivi karibuni, mkuu wa jeshi la Uganda, Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni mtoto wa Rais Museveni alisema kuwa wanamtafuta Bobi Wine, bila kufafanua iwapo kuna mashtaka yoyote rasmi dhidi yake.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Marekani yaishutumu Iran kwa kutoa madai ya uongo kuhusu meli yake ya kivita

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kamandi kuu ya kijeshi ya Marekani imelishutumu jeshi la Iran (IRGC) kwa kueneza madai ya uwongo kuhusu meli inayobeba ndege za kivita USS Abraham Lincoln.

    Kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, kamandi kuu ya kijeshi ya Marekani imeandika kuwa IRGC "kwa mara nyingine" imedai kuwa imeweza "kuzima" meli hiyo ya kivita.

    "Ifahamike: kikundi cha mashambulizi ya meli ya ndege ya Abraham Lincoln kinaendelea kuimarisha udhibiti kamili wa anga la Iran kutoka baharini," imesema taarifa hiyo.

    Marekani ilijiimarisha kijeshi Mashariki ya kati kabla ya mzozo huo.

    Mbali na Abraham Lincoln, meli kubwa zaidi ya ndege ya Marekani, USS Gerald Ford, pia inafanya kazi katika eneo hilo.

    Imebainika pia kwenye vyombo vya habari vya Marekani kuwa nchi hiyo inatuma majeshi ya ziada kwenye eneo la Ghuba, ikiwa ni pamoja na kikundi kinachojulikana kama kikosi cha kuvuka baharini (ARG) chenye wanajeshi wa majini wapatao 5,000.

    Meli ya mashambulizi ya majini USS Tripoli inatarajiwa kuungana na meli zilizopo tayari katika kambi hiyo ya kijeshi.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Mojtaba Khamenei yuko salama kiafya na anaongoza kikamilifu – Iran

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa masuala ya kigeni wa Iran, Abbas Araghchi, amesema katika mahojiano na Alaraby Aljadeed kwamba Mojtaba Khamenei yuko salama na mwenye afya njema" na "anaongoza kikamilifu."

    Itakumbukwa kwamba, Mojtaba hakujitokeza hadharani tangu uteuzi wake mnamo 8 Machi.

    Hotuba yake ya kwanza kwa umma ilirushwa na vyombo vya habari vya serikali mnamo 12 Machi, ikasomwa na mtangazaji.

    Araghchi amesema kuwa Iran inakaribisha “mpango wowote wa kikanda ambao utaweza kuleta mwisho wa haki wa vita,” na Bahari ya Hormuz “iko wazi kwa kila mtu isipokuwa meli za Marekani na washirika wake.”

    Aidha, Araghchi amesema kuwa “hakuna mpango maalum ulio mezani hadi sasa wa kumalizia vita.”

  7. Zaidi ya watu 100 wajeruhiwa katika saa 24 zilizopita - Israel

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya afya nchini Israel imetangaza kuwa watu 108 wamepelekwa hospitalini wakiwa na majeraha katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

    Kwa mujibu wa wizara hiyo,miongoni mwa majeruhi hao 96 walikuwa na majeraha madogo, wawili wako katika hali ya “wastani,” huku watu tisa wakiendelea kufanyiwa tathmini ya kitabibu.

    Tangu kuanza kwa mzozo huo, wizara hiyo inasema jumla ya watu 3,195 wamepatiwa matibabu hospitalini kutokana na majeraha yao.

    Kati yao, watu 81 bado wamelazwa hospitalini kufikia saa 07:00 GMT siku ya Jumapili.

    Wizara ya afya haijatoa taarifa kuhusu idadi ya vifo vilivyorekodiwa.

    Picha mpya zilizochukuliwa asubuhi hii zinaonyesha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya usiku kucha katika mji wa Holon, uliopo kusini mwa Tel Aviv.

    Katika picha hizo, gari moja linaonekana limepinduka, vifusi vimetapakaa eneo hilo, na kuna shimo kubwa katika upande wa jengo la makazi.

    Huduma ya dharura ya Magen David Adom (MDA) imesema ilitoa huduma ya kwanza kwa watu wawili waliokuwa katika eneo hilo wakiwa na majeraha madogo.

    Mwanaume mwenye umri wa miaka 80 alitibiwa kutokana na vipande vya kioo vilivyomjeruhi, huku mwanamke wa miaka 80 akitibiwa kutokana na kuvuta hewa ya moshi.

    Aidha, MDA imesema baadhi ya watu pia walipatiwa matibabu kutokana na mshtuko.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Iran yaapa kumfuatilia na kumuua waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jeshi la Iran IRGC limeapa kumfuatilia na kumuua waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya serikali.

    Shirika la habari la Iran, Mehr News Agency, linaripoti kuwa IRGC litaendelea “kumfuatilia na kumuua”.

    Aidha jeshi hilo pia linadai kuwa limeharibu maeneo kadhaa ndani ya Israel pamoja na vituo vitatu vya kijeshi vya Marekani katika eneo hilo wakati wa wimbi lake la 52 la mashambulizi.

    Wakati huo huo, watu 20 wamekamatwa katika mji wa Urmia nchini Iran wakituhumiwa kutuma taarifa za maeneo ya kijeshi, polisi na usalama kwa Israel.

    Kwa mujibu wa Tasnim News Agency, shirika la habari lenye uhusiano na IRGC, mitandao kadhaa ya watu wanaodaiwa kuwa mamluki wanaohusishwa na maafisa wa Israel imefungiwa.

    Watu hao 20 walikamatwa kufuatia amri ya mahakama, kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu wa jimbo la West Azerbaijan.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Mashindano ya mbio za magari F1 yaahirishwa kufuatia machafuko Mashariki ya kati

    xcv

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mashindano ya mbio za magari almaarufu langalanga nchini Bahrain na Saudi Arabia yameahirishwa rasmi, kwa mujibu wa waandaaji wa mbio hizo.

    Mashindano hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika tarehe 12 Aprili (Bahrain) na 19 Aprili (Saudi Arabia).

    Katika taarifa yake, Formula One imesema uamuzi wa kufuta mashindano hayo umetokana na hali inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Ingawa walijaribu kutafuta njia mbadala za kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kama kalenda yake inavyosema, hatimaye iliamuliwa kwamba hakutakuwa na mbadala wa mbio hizo.

    Kutokana na kusitishwa kwa mashindano hayo, sasa kutakuwa na pengo la wiki tano kati ya mashindano ya Japanese Grand Prix yatakayofanyika 27–29 Machi na Miami Grand Prix yatakayofanyika 1–3 Mei.

    Rais wa Fédération Internationale de l'Automobile (FIA), Mohammed Ben Sulayem, amesema:

    “FIA daima itazingatia usalama na ustawi wa jamii yetu na wafanyakazi wetu kwanza. Baada ya kutafakari kwa makini, tumechukua uamuzi huu tukizingatia jukumu hilo muhimu.”

    Pia unaweza kusoma:

  10. Israel yakiri kushambuliwa kwa makombora na Iran

    cvx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Shambulizi katika bandari ya Fujairah jana jumamosi

    Jeshi la Israeli linasema Iran imerusha makombora kuelekea Israeli.

    Inasema kwamba mifumo ya ulinzi inafanya kazi ili kuzuia tishio hilo na ujumbe wa tahadhari umetumwa kwa simu za mkononi katika maeneo yaliyoathiriwa.

    Israel imeonya umma kutoingia katika maeneo yaliyohifadhiwa hadi taarifa zaidi itakapotolewa.

    Shirika la Habari la Iran Fars, ambalo lina uhusiano na jeshi la Iran, linaripoti kwamba wimbi jipya la makombora limezinduliwa kutoka Iran huku kundi la wanamgambo wa Lebanon Hezbollah pia likirusha makombora au ndege zisizo na rubani kuelekea maeneo ya kaskazini mwa Israeli.

    Hayo yanajiri huku, wizara ya ulinzi ya Saudi Arabia ikitangaza kwamba ilidungua ndege 26 zisizo na rubani za Iran katika eneo lake, hasa karibu na mji mkuu Riyadh na katika maeneo ya mashariki mwa nchi.

    Mnamo alfajiri Falme za Kiarabu zilitangaza kwamba mifumo yake ya ulinzi wa anga ilikuwa ikijibu mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran.

    Hii inakuja baada ya moto mkali katika bandari ya Fujairah, kilipo kituo kikuu cha usafirishaji mafuta katika pwani ya mashariki ya nchi, kufuatia shambulio la ndege zisizo na rubani siku ya Jumamosi.

    Nayo, Bahrain ilitangaza kwamba ving'ora vyake vilikuwa vikilia na kuwahimiza wakazi kuelekea kwenye makazi ya karibu.

    Pia unaweza kusoma

  11. Marekani haiko tayari kufanya makubaliano na Iran - Trump

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa nchi yake haiko tayari kufanya makubaliano yoyote ya kumaliza vita vya sasa na Iran kwa sababu masharti yaliyowekwa hadi sasa hayatekelezeki.

    Trump alisema Iran ingependa kufikia makubaliano, lakini masharti hayo “hayajawekwa vizuri vya kutosha” kwa sasa, hivyo Marekani haiko tayari kuyakubali.

    Katika mahojiano na kituo cha habari cha Marekani, Trump alisema kwamba sehemu ya makubaliano yoyote ingehusisha ahadi ya Iran kuachana kabisa na mipango yake ya nyuklia, lakini hakutoa maelezo zaidi juu ya masharti hayo.

    Inavyyonekana Iran imekataa kufanya hivyo kama moja ya sharti katika makubaliano yoyote yatakayokubalika.

    Rais huyo pia alizungumzia usalama wa mlango wa baharini wa Hormuz, akisema baadhi ya nchi zimetangaza msaada wa kuhakikisha usafiri wa mafuta unaendelea bila usumbufu, ingawa hakutaja majina ya nchi hizo.

    Kauli hizo zinakuja huku vita baina ya Marekani, Israel na Iran ikiendelea kuibua mvutano mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati, na masuala yanayohusiana na usalama wa raia wa Marekani na maslahi ya mafuta duniani yakizidi kupewa uzito.

  12. Wananchi wa Congo-Brazzaville wanapiga kura leo kumchagua rais

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wananchi wa Jamhuri ya Congo (Brazzaville) wanapiga kura leo Jumapili katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kwa kiasi kikubwa kuongeza muda wa utawala wa kiongozi wa muda mrefu Denis Sassou Nguesso, mwenye umri wa miaka 82, kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

    Uchaguzi huo unafanyika huku upinzani ukiwa dhaifu na kukiwa na hali ya kutokuwa na mashaka makubwa kuhusu matokeo.

    Viongozi wawili maarufu wa upinzani bado wanashikiliwa gerezani, huku wengine wakiwa uhamishoni nje ya nchi. Baadhi ya vyama vya upinzani vimesusia uchaguzi huo vikisema mchakato wake hauna uaminifu.

    Zaidi ya wapiga kura milioni 3.2 wamesajiliwa kushiriki katika uchaguzi huo, ingawa wachambuzi na makundi ya kiraia wanatarajia idadi ya wapiga kura kujitokeza kwa uchache ikilinganishwa na karibu asilimia 68 iliyorekodiwa mwaka 2021, wakati Sassou Nguesso aliposhinda kwa kupata asilimia 88.4 ya kura.

    Kiongozi huyo alichukua madaraka mwaka 1979 katika taifa hilo la Afrika ya Kati linalozalisha mafuta, na ametawala karibu bila kukatizwa tangu wakati huo, isipokuwa kwa kipindi cha miaka mitano katika miaka ya 1990.

    Katika uchaguzi huu anakabiliwa na wagombea sita ambao hawajulikani sana, na hakuna anayeonekana kuwa mpinzani mkubwa, huku taasisi nyingi za uchaguzi zikidaiwa kutawaliwa na watu wanaoegemea chama tawala cha Congolese Labour Party.

  13. Idadi ya waliokufa kwenye mafuriko Kenya yafikia 62

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mvua kubwa na mafuriko nchini Kenya imefikia watu 62, wakiwemo watoto wanane, polisi wamesema.

    Mvua hizo zilianza kunyesha mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha mafuriko katika mji mkuu Nairobi pamoja na maeneo mengine ya nchi.

    Kwa mujibu wa taarifa ya polisi iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, jiji la Nairobi ndilo lililoathirika zaidi, likirekodi vifo 33.

    Wahudumu wa uokoaji walianza kuopoa miili kutoka kwenye maji ya mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Nairobi Jumamosi iliyopita, baada ya mafuriko ya ghafla yaliyotokea usiku kucha kusomba magari kadhaa na kusababisha usumbufu katika safari za ndege kwenye uwanja mkubwa zaidi wa ndege wa Afrika Mashariki.

    Taarifa iliyotolewa Jumapili iliyopita ilikuwa imeweka idadi ya vifo kuwa 42, lakini takwimu mpya zinaonyesha ongezeko la watu waliopoteza maisha.

  14. Marekani yawataka raia wake kuondoka katika nchi za Mashariki ya Kati

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imewataka raia wake kuondoka katika nchi kadhaa za Mashariki ya Kati kufuatia kuongezeka kwa mvutano wa kiusalama katika eneo hilo.

    Onyo hilo linakuja baada ya ubalozi wa nchi hiyo katika mji mkuu wa Baghdad kuwataka raia wa Marekani walioko Iraq kuondoka nchini humo mara moja, kufuatia shambulio la kombora lililopiga jengo la ubalozi huo mapema Jumamosi.

    Katika taarifa yake, ubalozi huo ulisema raia wa Marekani walioko nchini Iraq wanapaswa kufikiria upya uamuzi wao kutokana na tishio kubwa la makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran.

    Hatua hiyo inakuja wakati Iran imeanzisha mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati, ikilenga watu na rasilimali zingine zinazohusishwa na Marekani

    Katika hatua nyingine tofauti, Marekani pia imesema imewaamuru wafanyakazi wa serikali wasio wa dharura pamoja na ndugu wa wafanyakazi wa serikali kuondoka nchini Oman, kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Reuters.

    s