Wanawake watano wanaobadili maisha katika jamii zao na Afrika

Na Dinah Gahamanyi

BBC News Swahili

G

Chanzo cha picha, Faraja Kota Nyarandu/Twitter

Maelezo ya picha, Faraja Kotta Nyalandu

Wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo katika familia na jamii zao kwa ujumla. Katika makala hii tunawaangazia wanawake watano waliojitokeza, kwa kubuni shughuli zilizotambuliwa ambazo zimeweza kubadili maisha kwa namna moja au nyingine katika jamii zao na Afrika kwa ujumla.

Nora Magero

G

Chanzo cha picha, UNICEF

Maelezo ya picha, NORA MAGERO

Norah Magero,  mwanamke kutoka Kenya ni mtaalamu wa Uhandisi mitambo na  Nishati mbadala  kutoka Kenya  ambaye anazisaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, katika mazingira ya kukabiliwa na ubaguzi wa jinsia.

Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi Bi Magero ambaye ni muasisi wa Mkurugenzi mtendaji wa  Kampuni ya Drop Access, amekuwa akiongoza kampeni ya usawa katika haki za wanawake  za kupata elimu, nishati, mahitaji ya kimsingi  kulingana na Malengo ya kudumu ya maendeleo ya Umoja wa mataifa.

   Bi Magero ameweza kubuni kifaa cha  VacciBox -   ambacho ni friji inayotumia nishati ya jua ambayo inaweza kusafirishwa kwa baiskeli, pikipiki n ahata kubebwa , iki kurahisisha usambazaji wa chakula, vifaa vya tiba na madawa kwa usalama na kusafirishwa  kwenye jamii mbali mbali ambazo zimeathiriwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi  nchini Kenya.

Faraja Kotta Nyalandu

g

Chanzo cha picha, Faraja Kotta Nyalandu/Instagram

Maelezo ya picha, Faraja Kotta Nyalandu akifungua mkutano wa Mwaka wa Mtandao wa Elimu Tanzania,- ni muasisi na Mkuregenzi mkuu wa taasisi ya Shule Direct inayotoa elimu kwa njia ya mtandao Tanzania na Afrika

Faraja Kotta, ni mmoja wa wanawake  wa Kitanzania, anayeaminiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu hususan ni katika utoaji wa elimu ya  mtandao  kwa vijana wa kike. Mwanamke huyu ambaye anashikilia taji la urembo nchini Tanzania la mwaka 2004, ni muasisi na Mkurugenzi mtendaji wa Shule Direct, kampuni inayobuni maudhui ya kidigitali  ya kielimu kwa ajili ya vijana wa  Tanzania na  kote Afrika kwa njia ya wavuti na simu za mkononi.

Mwaka 2016 alitunukiwa Tuzo ya mwanamke anayeongoza katika teknolojia barani Afrika kutokana na kazi yake ya Shule Direct, na Mwaka huo huo alitunukiwa tuzo la Uongozi  nchini Tanzania, kitengo cha mwanamke maarufu wa mwaka.

Christelle Kwizera  

g

Chanzo cha picha, Christelle Kwizera

Maelezo ya picha, Christelle Kwizera
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Christelle Kwizera, 25, ni kijana wa Kinyarwanda Mhandisi Mitambo na mjasiliamali wa Kijamii. Katika mwaka 2014, Christelle alianzisha kampuni yake inayoitwa  Water Access Rwanda, inayotoa huduma ya usafishaji maji yanayotumiwa.

Kampuni ya Bi Kwizera imetoa maji safi kwa zaidi ya Wanyarwanda 100,000 kupitia mtandao wa mashimo ya kuhifadhia maji (boreholes) 95  pamoja na mfumo wa usafishaji maji  INUMA.

 Water Access Rwanda ndio kampuni pekee ya Rwanda ambayo imewahi kutunukiwa  tuzo la ujasiliamali  la Afrika. Christelle pia alitambuliwa kama  Mwanamke mjasiliamali wa mwaka  2019  mjini  Paris na kampuni ya  INCO.

 “Tunatoa maji salama yaliyochujwa kwa bei nafuu. Hii husaidia upatikanaji wa mud ana fedha ambazo zinaweza kutumiwa kwa ajili ya shughuli nyingine za kuongeza kipato , kuwawezesha watoto kupata muda zaidi wa kuangazia masomo na wanawake kutumia muda zaidi katika shughuli za kiuchumi na kisiasa kiuchumi na hivyo kuwezesha mafanikio kuelekea  maendeleo ya kudumumu’, alisema Bi Kwizera katika mahojiano na jarida la Vital Voices.

''Mama Police''

g

Chanzo cha picha, UN news

Maelezo ya picha, Sejenti Milly Labol, anafahamika kwa kazi yake kama ‘Mama Police’

Katika kitengo cha polisi cha kuwalinda watoto nchini Uganda anapatikana  Sejenti Milly Labol, al maarufu  ‘Mama Police’  kutoka wilaya ya  Namayingo , mashariki mwa  Uganda.

Ingawa jukumu la kuwalinda watoto na watoto dhidi ya unyanyasaji  ni jukumu lake , Mama police amekukuwa akiwahamasisha wadau wengine wa masuala ya watoto kama vile Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa  UNICEF na wengine kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kuwa na uelewa wa  vitendo vya kiutamaduni vinavyowanyanyasa wanawake na watoto.

‘‘Mama police’’, amesifika na kutambuliwa na Shirika la watoto la Umoja wa mataifa Unicef kama mmoja wa wanawake walio mstari wa mbele  katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa watoto katika jamii yake.

Nancy Tembo

g

Chanzo cha picha, Nancy Tembo/Twitter

Maelezo ya picha, Nancy Tembo

Nancy Tembo , ni Waziri wa misitu na Maliasili wa Malawi, ambaye alichaguliwa kama mbunge katika miaka ya 2004 na 2019.  

Akiwa katika wadhifa wake wa sasa , amekuwa mtari wa mbele katika kuhakikisha misitu ya  Malawi inarejeshwa kwa kuwahamasisha watu kuacha kutumia mkaa – na badala yake kutumia majiko yanayopiga kwa haraka  au majiko ya gesi, ili kurejesha misitu .

Katika tukio la hivi karibuni la upandaji wa miti mjini Lilongwe alielezea  athari zinazosababishwa na ukataji wa miti : “Sote tunajitaki miti karibu kwa kila kitu tunachokifanya kila siku. Ukweli ni kwamba, tunahitaji miti kuliko miti inavyotuhitaji sisi .”