Ajali 7 za ndege mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Siku mbili hivi, ajali mbili za ndege zimetokea. Ndege ya jeshi aina ya C-130 Hercules iliyobeba watu 125 imeanguka Colombia na kusababisha vifo vya watu 34. Huko New York, ndege ya Air Canada AC8646 iligongana na gari la zimamoto kwenye uwanja wa ndege wa LaGuardia Jumapili usiku, ikaua marubani wawili na kujeruhi watu kadhaa wengine.
Hii ni kuendelea kwa mlolongo wa ajali za anga zinazohusisha vifo vingi. Simanzi nzito ilienea India baada ya ajali mbaya ya ndege ya Air India, iliyokuwa ikielekea London na kubeba abiria 242. Ndege hiyo ilianguka Alhamisi, Juni 12, 2025, muda mfupi baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Ahmedabad, magharibi mwa India.
Maafa haya yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 200, na taarifa za awali zikibainisha kuwa miili 204 imepatikana. Idadi ya walio hai na waliokuwa chini wakati wa ajali bado haijafahamika, huku uchunguzi ukiendelea kubaini ukubwa kamili wa janga hilo. Ndege hiyo ilianguka kwenye jengo lililokuwa likitumiwa kama makazi na hospitali, huku simulizi za waathiriwa zikibainisha baadhi ya waliopona walionusurika kwa kuruka kutoka dirishani ghorofa ya pili.
Kati ya abiria, walikuwa raia 169 wa India, Waingereza 53, Wareno 7, na Mcanada 1. Ajali hizi za hivi karibuni zinaongeza kwenye orodha ndefu ya matukio mabaya katika historia ya usafiri wa anga, zikikumbusha ulimwengu hatari zilizopo licha ya maendeleo makubwa katika sekta hii.
Ukiacha ajali hizi, hizi ni miongoni mwa ajali tano za ndege mbaya zaidi zilizotokea duniani, kulingana na mitandao mbalimbali ikiwemo Cartoskills na PTC News.
1. Pan Am Flight 1736 na KLM Flight 4805 – Vifo 583
Janga hili linakumbukwa kama ajali mbaya zaidi katika historia ya usafiri wa anga, ilitokea Tenerife, visiwa vya Canary mnamo Machi 27, 1977. Ndege mbili za Boeing 747 ziligongana kwenye barabara ya kurukia ndege katika Uwanja wa Ndege wa Los Rodeos (sasa Uwanja wa Ndege wa Tenerife North) kwenye kisiwa cha Hispania cha Tenerife, Visiwa vya Canary.
Tukio hili lilisababisha vifo vya watu 583. Kutokana na mwingiliano tata wa sababu mbalimbali, ikiwemo ushawishi wa shirika, hali ya mazingira, na vitendo visivyo salama vilivyopelekea ajali hii, maafa ya Tenerife yamekuwa mfano wa kitabu cha kiada kwa ajili ya kukagua michakato na mifumo inayotumika katika uchunguzi wa ajali za anga na kuzuia ajali.
2. Japan Airlines Flight 123 – Vifo 520
Ndege ya Japan Airlines Flight 123 ilikuwa safarini kutoka Uwanja wa Ndege wa Haneda, Tokyo, kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Osaka, Japan. Mnamo Jumatatu, Agosti 12, 1985, ndege ya Boeing 747SR iliyokuwa ikifanya safari hii ililipuka ghafla dakika 12 baada ya kuruka. Dakika 32 baadaye, ndege hiyo ilianguka kwenye milima miwili ya Mlima Takamagahara huko Ueno, Wilaya ya Gunma, kilomita 100 (maili 62) kutoka Tokyo, karibu na Mlima Osutaka.
3. Saudi Arabian Flight 763 na Kazakhstan Airlines Flight 1907 – Vifo 349

Chanzo cha picha, Getty Images
Hii ndiyo ajali mbaya zaidi ya ndege mbili kugongana hewani. Ilitokea katika anga ya kijiji Charkhi Dadri, magharibi mwa New Delhi, India tarehe12 Novemba 1996.
Ndege zilizohusika zilikuwa Saudi Arabian Airlines Boeing 747-100B iliyokuwa ikitoka Delhi kwenda Dhahran, Saudi Arabia, na Kazakhstan Airlines Ilyushin Il-76 iliyokuwa ikitoka Chimkent, Kazakhstan, kwenda Delhi.
Ajali hiyo iliua watu wote 349 waliokuwa ndani ya ndege zote mbili, na kuifanya kuwa ajali mbaya zaidi ya kugongana hewani duniani, ajali mbaya zaidi ya anga kutokea nchini India, na ajali ya tatu mbaya zaidi ya ndege katika historia ya usafiri wa anga.
4. Turkish Airlines Flight 981 – Vifo 346

Chanzo cha picha, Getty Images
Turkish Airlines Flight 981 ilikuwa inafanya safari ya mara kwa mara kutoka Uwanja wa Ndege wa Istanbul Yesilköy kwenda Uwanja wa Ndege wa London Heathrow na kituo cha kati kilikuwa Paris, Orly Airport. Mnamo Machi 3, 1974, ndege aina ya McDonnell Douglas DC-10 iliyokuwa ikifanya safari hiyo ilianguka katika msitu wa Ermenonville nje ya Paris, na kuua watu wote 346 waliokuwemo ndani.
Wakati huo, ilikuwa ajali mbaya zaidi ya ndege katika historia ya usafiri wa anga. Bado inabaki kuwa ajali ya nne mbaya zaidi ya ndege katika historia ya usafiri wa anga, ya pili mbaya zaidi bila manusura, na ajali mbaya zaidi ya ndege moja bila manusura, na ajali ya pili mbaya zaidi ya anga barani Ulaya.
5. Air India Flight 182 – Vifo 329

Chanzo cha picha, Getty Images
Air India Flight 182 ilikuwa ikifanya kazi kwenye njia ya Vancouver–Toronto–Montreal–London–Delhi. Mnamo Juni 23, 1985, ndege ya Boeing 747-237B iliyokuwa ikifanya safari hiyo ilisambuliwa kwa bomu ikiwa kwenye urefu wa futi 31,000 (mita 9,400). Ilianguka katika Bahari ya Atlantiki ikiwa katika anga ya Ireland.
Ilikuwa ndege ya kwanza kubwa ya 747 kulipuliwa. Jumla ya watu 329 waliuawa, ikiwemo raia 268 wa Canada, raia 27 wa Uingereza, na raia 24 wa India. Tukio hilo lilikuwa mauaji makubwa zaidi katika historia ya Canada.
Ilikuwa shambulio baya zaidi la kigaidi lililohusisha ndege hadi pale mashambulizi ya Septemba 11, 2001 yalipotokea. Pia unatajwa kama mlipuko mbaya zaidi wa ndege.
Tukio la kulipuliwa kwa Air India 182 kulitokea sambamba na ulipuaji wa Uwanja wa Ndege wa Narita. Wachunguzi wanaamini kulikuwa na uhusiano katika mipango ya matukio hayo miwili.
6. Malaysia Airlines Flight MH17 - Vifo 298
Ndege ya Malaysia Airlines Flight MH17 ilianguka mwaka 2014 baada ya kushambuliwa wakati ikielekea Amsterdam kutoka Kuala Lumpur, Malaysia. Ajali hii ilitokea kwenye anga la Ukraine ambalo lilikuwa likishuhudia mgogoro wa kijeshi kati ya majeshi ya serikali na waasi.
Ndege hiyo ilikuwa na watu 298 ndani, wakiwemo raia wa Uholanzi, Malaysia, Australia, Ujerumani, Uingereza, Ujerumani na mataifa mengine, ambao walipoteza maisha.
Ajali ya MH17 imekuwa mojawapo ya ajali mbaya zaidi za ndege zinazohusiana na vurugu za kivita, ikitolewa kama kielelezo cha hatari zinazoweza kutokea kwenye mizozo.
7. Iran Air Flight 655 - Vifo 290
Ndege ya abiria ya Iran Air Flight 655 ilianguka mwaka 1988 katika Bahari ya Persian Gulf na kuua watu wote baada ya kushambuliwa kimakosa na Marekani.
Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Dubai kutoka Tehran na ilibeba abiria 290, wote waliokuwa raia, ikiwemo wanawake, watoto, na familia mbalimbali.
Kosa hili la kijeshi liliibua huzuni na hasira kubwa duniani, huku kusababisha mazungumzo zaidi kati ya Iran na Marekani.
Ajali ya Iran Air 655 inachukuliwa kama mojawapo ya ajali mbaya zaidi za anga zinazohusiana na vurugu za kivita, na ilionyesha jinsi makosa ya kijeshi yanaweza kuathiri raia wasio na hatia. .














