Kwa nini Afrika inakabiliwa na uhaba wa mafuta licha ya utajiri wa bidhaa hiyo muhimu?

    • Author, Marco Oriunto
    • Akiripoti kutoka, London
    • Author, Makuochi Okafor
    • Akiripoti kutoka, Lagos
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kadri vita vinavyoendelea nchini Iran, mataifa mengi barani Afrika yanaanza kuhisi athari zake kwa viwango tofauti.

Baadhi ya mataifa barani Afrika yanakabiliwa na changamoto za kupanda kwa bei ya mafuta na kuvurugika kwa usafirishaji, huku mengine yakipata fursa mpya za biashara kutokana na mabadiliko ya njia za meli.

Nigeria: Tajiri wa mafuta, lakini bado inabanwa

Nigeria ni mzalishaji wa pili wa mafuta barani Afrika baada ya Libya. Ongezeko la bei ya mafuta ghafi limeifanya serikali kuashiria uwezekano wa kuongeza uzalishaji ili kusaidia kukidhi mahitaji ya kimataifa.

Hata hivyo, faida hizo huenda zisifike kwa wananchi wa kawaida. Sababu kuu ni ukosefu wa uwezo wa ndani wa kusafisha mafuta. Nigeria husafirisha mafuta yake ghafi nje ya nchi ili yasafishwe kuwa bidhaa kama petroli na dizeli, kisha hununua tena kwa bei ya soko la dunia. Ni hali ambayo nchi nyingi Afrika zinazochimba mafuta zinakabiliwa na changamoto hizo.

Wakati huo huo, usumbufu katika mlango bahari wa Hormuz umeathiri usafirishaji wa mafuta, na hivyo kusababisha bei kupanda hata ndani ya Nigeria na mataifa mengine Afrika.

"Mara tu bei ya petroli inapopanda kimataifa, gharama za usafiri huongezeka kila mahali," anasema Dumebi Oluwole, mwanauchumi kutoka Lagos.

Kwa upande wake, Morounmubo Akodu, mfanyabiashara mdogo, anasema: "Bei ya mafuta imeongezeka maradufu au hata tatu. Ninalazimika kufanya kazi pale tu inapobidi ili kudhibiti gharama."

Mbali na mafuta, gharama za chakula pia zinatarajiwa kupanda, na mfumuko wa bei kuongezeka. Hivyo, ingawa serikali inaweza kuongeza mapato kutokana na mauzo ya mafuta, wananchi wengi wanakabiliwa na ongezeko la gharama ya maisha.

Mbali na gharama za mafuta, chakula kinaweza kuwa ghali zaidi na mfumuko wa bei kuwa mbaya zaidi na kusababisha gharama zote za maisha kuwa za juu.

Wakati serikali inaweza kupata zaidi kutokana na mauzo ya mafuta, Wanigeria wengi wanakabiliwa na gharama kubwa za maisha kwa siku zijazo.

Misri: Mfereji wa Suez katika shinikizo

Nchini Misri, athari zinaonekana moja kwa moja kupitia sekta ya usafirishaji.

Mfereji wa Suez ni njia muhimu kwa meli zinazobeba mafuta na bidhaa kati ya Ghuba na Ulaya. Hata hivyo, tangu kuanza kwa mapigano, kampuni nyingi za usafirishaji zimeelekeza meli zao mbali na mlango-bahari Hormuz na Bahari Shamu kutokana na vitisho vya mashambulizi ya makombora na droni.

Hatua hii imepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya meli zinazopita katika Mfereji wa Suez, na hivyo kupunguza mapato ya Misri. Aidha, gharama za uagizaji zimeongezeka, jambo linalosababisha kupanda kwa bei za bidhaa ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa uchumi Dumebi Oluwole, thamani ya sarafu ya Misri imeshuka kwa takriban asilimia saba hali inayochochewa na kupungua kwa shughuli katika mfereji huo muhimu.

"Pauni ya Misri imepoteza takriban 7%," anasema mwanauchumi Dumebi Oluwole.

"Hiyo ni kwa sababu Mfereji wa Suez, ambao ni njia kuu ya usafirishaji wa mafuta ghafi na bidhaa nyingine nyingi kwenda Ulaya, kimsingi umezuiwa."

Afrika Kusini: Fursa mpya, lakini kwa tahadhari

Kwa upande wa kusini mwa bara, hasa nchini Afrika Kusini, mabadiliko haya yameleta fursa mpya za kiuchumi.

Kampuni kubwa za usafirishaji kama Maersk na Hapag-Lloyd zimetangaza kuanza kuelekeza baadhi ya meli zao kupitia Cape of Good Hope ili kuepuka maeneo hatarishi ya mlango bahari wa Hormuz na Bahari ya Shamu.

Matokeo yake, bandari za kusini mwa Afrika ikiwemo Cape Town, Durban, Maputo na Dar es Salaam zinashuhudia ongezeko la shughuli za meli.

Kwa mujibu wa Timothy Walker, mtafiti wa masuala ya usalama, njia hizi mpya ndefu zitaongeza shinikizo kwa miundombinu ya bandari katika ukanda huo.

Takwimu kutoka Baraza la Biashara na Viwanda la Cape zinaonyesha kuwa Bandari ya Cape Town ilishuhudia ongezeko la asilimia 112 la meli mwanzoni mwa mwezi Machi.

Hata hivyo, changamoto bado zipo. Jacques Moolman anaeleza kuwa, licha ya fursa katika huduma za meli kama usambazaji wa mafuta, ukarabati na vifaa vya baharini, bado kuna mapungufu ya miundombinu.

"Wakati kuna uwezekano wa fursa za kibiashara katika uhifadhi, ukarabati wa meli na vifaa vya baharini, kuna vikwazo vya miundombinu," anasema Jacques Moolman, Rais wa Rais wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Cape.

Mamlaka ya Kitaifa ya Bandari ya Transnet (TNPA), chombo kinachomilikiwa na serikali ambacho kinamiliki na kusimamia bandari nane za kibiashara za Afrika Kusini, ilithibitisha mipango ya kujenga kizimba kipya cha kuelea mjini Cape Town. na kuzindua mfululizo wa maboresho ili kuimarisha sekta ya ndani ya ukarabati wa meli.

Pamoja na hayo, taswira ya uchumi wa Afrika Kusini inabaki kuwa ya mchanganyiko.

Nchi hiyo inaagiza sehemu kubwa ya mafuta yake, hivyo kupanda kwa bei za kimataifa na ucheleweshaji wa usafirishaji vitaathiri watumiaji na biashara hata kama sekta ya bahari itaendelea kunufaika.

Tanzania na Kenya wameathirika vipi?

Wakati hofu ya uhaba wa mafuta ikiendelea miongoni mwa raia wa Kenya na Tanzania serikali za nchi hizo mbili na wadau wa sekta hiyo zimewahakikishia wananchi wao kuwa hali ya upatikanaji wa bidhaa hiyo ni wa kuridhisha na hakuna uhaba.

Hata hivyo wafanyibiashara wa nchi hizo mbili wanakadiria hasara kubwa kutokana na kufutwa kwa baadhi ya ndege na ucheleweshaji wa bidhaa zinazosafirishwa kupitia meli.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid