Je, Iran inaweza kutengeneza silaha za nyuklia?

Chanzo cha picha, Getty Images/BBC

Muda wa kusoma: Dakika 4

Hifadhi ya madini ya urani ya Iran, bado ni suala tete katika mgogoro wa Iran na Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa Iran iko tayari kuipa Marekani madini hayo vita hivyo vikimalizika.

Siku ya Jumatatu, naibu Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Saeed Khatibzadeh alikanusha semi hizo na kuiambia shirika la habari la AP kuwa hilo "halikubaliki".

Pande hizo mbili zikiendelea kufanya mazungumzo, suala la madini ya urani huenda ukaleta utofauti kati yao.

Kwa nini madini haya ya urani yana umihimu mkubwa hivyo?

Madini ya urani ni nini?

Haya ni madini yanayopatikana ardhini.

Madini haya huwa na isotopu mbili U-238 na U-235.

99% ya urani asilia ni U-238 ambayo haina tanuri ya nyuklia. Takriban 0.7% ya U-235 ndiyo inauwezo wa kutoa nishati ya nyuklia.

Ili madini ya urani yawe na maana, aina ya U-235 lazima itumiwe kwa wingi katika mchakato wa kuirutubisha.

Urani hubadilishwa kwanza kuwa gesi, na kuwekwa kwenye mashinepewa.

Mashine hiyo huzungusha madini hayo na U-238 huzunguka kwa kutoka nje ya mzunguko, huku U-235 ambayo ni nyepesi hubakia karibu na kitovu cha mashine hiyo.

Hatua hii huitenganisha U-235 ambayo ndiyo muhimu sana kutoka kwa U-238.

Chanzo cha picha, Getty Images

Tofauti kati ya urani ambayo hutumika katika vinu vya nyuklia na silaha za nyuklia

Viwango fulani vya urutubishaji vinaifanya urani kufaa katika matumizi mbalimbali.

Urani hurutubishwa kwa kiwango cha chini cha 3% hadi 5% ya U-235, na hii hutumika katika mashine za kibiashara na huzalisha nishati ya nyuklia,kiwango hiki hakitoshi kutengeneza silaha za nyuklia.

Urani uliorutubishwa kwa kiwango cha juu cha hadi 20% au zaidi, ndiyo hutumika katika vinu vya utafiti, na zile ambazo hutumika kwa silaha za vita hurutubishwa hadi kiwango cha 90%.

Katika makubaliano yaliyoafikiwa mwaka wa 2015, na mataifa sita yenye nguvu duniani, China, Ufaransa,Ujerumani,Urusi,Marekani na Uingereza, Iran iliekewa vikwazo vya kurutubisha urani hadi kiwango cha 3.67%.

Makubaliano hayo pia yalisema hifadhi ya urani ya Iran isipite kilo 300, na kuweka viwango vya mashinepewa za kutumia na kupiga marufuku urutubishaji wa chini ya ardhi ambao ulikuwa unafanywa na Iran.

Ila mwaka wa 2018, Trump alijiondoa katika makubaliano hayo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mbona kiwango hiki cha urutibishaji ni muhimu?

Kiwango cha juu cha urutubishaji huongeza uwezo wa kutumika katika silaha za nyuklia.

Kufikia urutubishaji wa kiwango cha 20% ni hatua kubwa, kwani inahitaji uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kijeshi kufikia hatua hii, na pia madini hayo hupitishwa katika hatua kadhaa ambayo huchukua muda na juhudi nyingi.

Ila kurutubisha urani kutoka 20% hadi 90% huchukua hatua kidogo.

Hii inamaanisha urani iliyorutubishwa kwa kiwango kikubwa, inaweza kubadilishwa kuwa silaha kwa haraka sana.

Iran ina kiwango kipi cha urani?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa sasa hatma ya hifadhi ya urani ya Iran haijulikani.

Katika mwanzo wa vita Iran ilikuwa na kilo 440 ya urani ambayo imerutubishwa kwa kiwango cha 60% kulingana na maafisa wa Marekani. Madini hayo yanaweza kurutubishwa haraka na kufikia 90%, kiwango kinachohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.

Iran pia ina kilo 1000 ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha 20% na kilo 8500 iliyorutubishwa kwa kiwango cha 3.6%.

Kiwango kikubwa cha urani ambacho kinaweza kutumika kutengeneza silaha za nyuklia kimehifadhiwa eneo la Isfahan.Hii ni mojawapo ya vituo vitatu chini ya ardhi ambavyo vililengwa katika mashambulio ya Marekani na Israel mwaka uliopita.

Aidha haijulikani kabisa, ambako hifadhi nyingine za urani zilipo.

Tehran inasemekana kukataa pendekezo la kusitisha urutubishaji wa madini ya urani kwa miaka 20 ila wakapendeza kusitisha hatua hiyo kwa muda wa miaka mitano pekee.

Tehran pia ilikataa kuipa Marekani, hifadhi yake ya kilo 440 ya urani iliyorutubishwa kwa 60%, na wanataka kuyeyusha madini hayo.

Mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki (IAEA) Rafael Grossi aliliambia shirika la habari la AP kuwa iwapo kiwango hiki cha madini ya Urani ya Iran yataendelea kurutubishwa zaidi, yanaweza kutengeneza mabomu 10 ya nyuklia.

Je, Iran inatengeneza silaha ya nyuklia?

Iran inasisitiza kuwa vituo vyake vya nyuklia ni vya matumizi ya amani pekee, na shirika la IAEA limesema halijaona ushahidi wa kuwepo kwa mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Uzalishaji wa urani yenye kiwango cha juu kinachoweza kutumika kutengeneza silaha ni hatua moja tu katika uundaji wa bomu la nyuklia. Bomu kamili pia linahitaji hatua nyingine ikiwemo kubuni na kuunganisha kichwa cha kivita pamoja na kutengeneza mfumo wa kulifikisha au kulirusha katika eneo husika la vita.

"Iran ilikuwa imepiga hatua fulani ya kubuni vichwa vya nyuklia hadi mwaka wa 2003, ilipoonekana kusitisha mpango huo," anaeleza Patricia Lewis, mtaalamu huru wa udhibiti wa silaha.

Hata hivyo, anaongeza kuwa "baada ya kufeli kwa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 na kuendelea kushindikana kwa mazungumzo ya kufikia makubaliano mapya, inawezekana Iran imeamua kuanza tena kuendeleza mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia."

Tathmini iliyofanywa mwezi Mei mwaka wa 2025 na shirika la ujasusi la Marekani la Defense Intelligence Agency, ilisema kuwa Iran inaweza kuzalisha urani wa kiwango cha kutengeneza silaha moja ya nyuklia kwa kipindi cha wiki moja.

Hata hivyo, tathmini hiyo pia ilieleza kuwa Iran "kwa hakika haitengenezi silaha za nyuklia" kwa sasa, ingawa imechukua hatua ambazo zinaweza kuiweka katika nafasi ya kufanya hivyo iwapo itaamua.