WARIDI WA BBC:‘Najuta kwenda Saudia Arabia kufanya kazi za nyumbani’

Na Anne Ngugi

BBC Swahili,Nairobi

Raha kugeuka kuwa karaha.Ndio muhtasari unaoweza kubeba matumaini  ya Hellen Ndege yaliyoyeuka pindi alipokanyaga ardhi ya Saudi Arabia .

Mpango  wake ulikuwa rahisi sana-kwenda nchi hii ya kigeni kufanya kazi za nyumbani   kwa miaka ili kuboresha maisha yake.Tatizo ni kwamba kitumbua kilipoingia mchanga,haikuwa rahisi yeye kurejea nyumbani kama alivyotamanI.Tayari alikuwa amejinasa kwa minyororo ya mikataba  alioitia saini kabla ya kuanza safari yake .

Hellen  aliwasili Saudia mwaka wa 2019 na misheni yake kwa kauli yake mwenyewe ilikuwa hii:

‘Mimi nimepitia  shida nyingi sana kabla sijaamua kusafiri hadi nchi ya Saudia kutafuta riziki .

Nilikuwa nimeacha shule nikiwa darasa la sita na nilihisi kwamba njia pekee ya kufaulu pamoja na kuisaidia familia yangu  kumaliza umaskini ni  kusafiri kwenda  nje ya nchi ”

 Kwanini alikubali kusafiri Saudi Arabia ?

Fursa  ya kwenda Saudi Arabia ilipochipuka hakufikiria mara mbili kuhusiana na yale yaliokuwa mbele . Anasema kwamba alikuwa ameyasikia masaibu mengi ambayo yalikuwa yamewapata baadhi ya wasichana wa kazi za nyumbani  waliokuwa wamesafiri katika nchi tofauti mashariki ya kati , ila kwake alikuwa na matumaini kwamba angeyavumilia yote ilimradi aafikie ndoto za kuaga umasikini .

Kati ya siku ambazo hawezi kuzisahau ni tarehe 9 mwezi Februari mwaka wa 2019 ambako alijificha wakati akiondoka kusafiri Saudia ili mtoto wake wa kiume  asimuone akiondoka .

Mama huyu alihisi uchungu kumuacha mtoto wake wakati huo akiwa na miaka minne , ila kimoyomoyo aliona miaka miwili kama muda mfupi kuafikia malengo yake .

Baada ya kuwasili Saudi Arabia Hellen anasema kwamba yeye alipokewa na baba na mama kutoka jamii iliyokuwa imempa kandarasi ya kufanya kazi  na moja kwa mmoja kuelekea nyumbani kwao .

Kulingana na mwanadada huyu ,japo alikuwa amefanya kazi za nyumbani nchini Kenya kwa miaka zaidi ya 10 alianza kuwa na changamoto kuanzia siku ya kwanza  kwa sababu ya changamoto ya  lugha na mawasiliano  yakawa magumu  na mwajiri wake .Pia joto lilikuwa kali  na kwa sababu ya kutozoea hali hiyo ilipata usumbufu mkubwa sana .

 Imani yake kwamba mambo yangeboreka ilisalia kuwepo na  akapiga moyo kondo kuyafumbia macho mambo hayo akifikiri ni madogo sana kumzuia kutimiza malengo yake .

Hata hivyo siku  zilivyozidi kwenda aligundua kwamba kazi zilikuwa ni nyingi mno na kila siku alikuwa akilazimika kuamka  asubuhi na mapema na kulała nyakati za  usiku wa manane mara nyingi saa kumi za asubuhi .

 

Kando na hayo kulikuwa na kazi nyingine za kuhakikisha kwamba ameandaa mapishi kwa wakati , anadai kwamba wenye nyumba walikuwa hawaingii jikoni na ilikuwa kazi yake kulingana na kandarasi aliyotia sahihi .

Hellen anasema kwamba baada ya miezi 9 ya kwanza kufanya kazi alihisi kwamba wakati ulikuwa umefika kwake kurudi nyumbani - Kenya , lakini kikwazo kikawa  ni kandarasi yake .

Jaribio lake la kutoroka liligonga mwamba kwani  kwa sababu kwa mujibu wa masharti ya mkataba wake ,lazima angefanya kazi kwa mwajiri yul kwa miaka miwili . Dhulma dhidi yake zilikuwa zimekuwa jambo la kawaida na kwa uvumilivu aliendelea kufanya kazi .

Hellen anasema kwamba wakati alipoanza kazi walikuwa wamekubaliana na mwajiri wake  kwamba angepokea karibu dola mia mbili hamsini kila mwezi  au Riyal  mia tisa kila mwezi .Mwanadada huyu anasema kwamba aliamua kuhakikisha kwamba ametuma Riyal mia  tano nyumbani kwa sababu ya mahitaji ya mtoto wake  na  kisha Riyal mia nne zilizosalia aliamini tajiri wake  angemuekea  akiba hadi wakati angerudi nchini Kenya .

Kwa muda anasema mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 29 mzaliwa wa magharibi mwa Kenya anasema  alivumilia kila hali ya kazi na pia maisha ya kufanya kazi bila kupumzika .

 

Unyanyasaji wa Kingono

Hellen anakumbuka tukio la kuogofya siku moja mbapo mwajiri wake mama mwenye nyumba alikuwa ametoka na wanawe kwenda kujivinjari kama ilivyokuwa ada yao katika siku maalum .Baba mwenye nyumba alirejea nyumbani ghafla na alipoingia katika nyumba aliifunga milango yote .

 Alimtaka amuandalie kahawa jikoni na alipokuwa akifanya hivyo alimshtukiza na kumshika kwa nguvu ,mapambano ya dakika kama thelathini yalitokea huku lengo la mwajiri wake huyo likiwa kumdhullumu kimapenzi .Hellen  alijaribu kupiga ukemi lakini alifahamu hilo halingemsaidia kwani jumba lenyewe lilikuwa kubw ana hakuna aliyweza kumsikia .

Afueni yake ilitokea wakati simu ya nyumba alipopigwa na mwajiri wake akaacha kwa muda kumshika kwa nguvu na ndipo alipopata nafasi ya kukimbia hadi bafuni alikojifungia hadi mama mwenye nyumba na watoto wake waliporejea .

‘Kisa hiki kilinisukuma kupigana kurudi nyumbani kwa vyovyote vile , niliogopa kumueleza mtu yeyote kuhusiana na yaliyojiri.Hofu yangu kuu ilikuwa kwamba hakuna ambaye angeniamini na nilihofu kwamba ningesingizwa lawama kwa kilichotokea .Niliamua kutafuta ajenti walionileta hadi huko’

Baada ya hapo Hellen alianza kutafuta kila mbinu kupiga simu nyumbani katika juhudi za  kutaka ujumbe uwafikie mawakala wake nchini Kenya  kwamba yeye alikuwa hana amani na alitamani arejee kutokana na tishio la dhuluma dhidi ya maisha yake .

Mchakato wa kurudi Kenya ulianza wakati  mawakala wake kwa upande wa nchi ya Saudi Arabia walianza mawasiliano na mwajiri wakitaka aheshimu kandarasi yake ambayo ilikuwa inakaribia kufika mwisho wake baada ya miaka miwili .Hellen anasema kwamba hakuwahi kufunguka kuhusiana na jaribio ya ubakaji kwa uwoga .Anaongeza kwamba alichotamani sana wakati huo ni kurudi nyumbani

Tarehe 6 mwezi mei mwaka huu Hellen aliraushwa mapema na tajiri wake na kuelezwa kwamba  alifaa kufunga safari ya kurudi  Kenya , aliambiwa kwamba  tiketi yake ya ndege ilikuwepo na hata kuwa na muda wa kujitayarisha . 

Kinachompa machungu  sana kando na mateso mengi aliyoyapitia akiwa huko ni kwamba kati ya pesa takriban  Riyal alfu kumi na tatu ambazo  mwajiri wake alikuwa amemuwekea kama akiba yake kutoka kwa mshahara wake wa kila mwezi mwanadada huyu anadai kwamba tajiri wake aliamua kumlipa nusu ambayo ni Riyal 6500.Jasho lake la miaka miwili aliyojinyima mengi halikuzaa matumaini aliyoyabeba akienda nchini humo .

Hata hivyo  Hellen anafuraha kwamba alirudi  akiwa mzima wa afya .

Anasema kwamba changamoto kuu inayowakabili wasichana wengi wanaokwenda uarabuni  kwa kazi za ndani ni ukosefu wa habari kuhusiana na jinsi ya kujilinda wakati shida inapowapata  na hasa kwa kuwa hawaelewi mazingira wanayoyaishi pamoja na mila na desturi za huko .

 Cha pili  anasema kwamba wengi wa waajiri wa huko wanawaona wasichana kama Hellen kama watumwa , hii inatokana na kwamba wanalipa pesa nyingi kupitia mawakala ili kuajiri wasichana wa kazi za ndani kutoka nchi mbali mbali Afrika na pia bara Asia

Kwa sasa Hellen ameanza biashara ya uuzaji dagaa viungani mwa mji wa Nairobi na anasema kwamba anatosheka na kidogo anachopata  .