Asim Munir: Kutoka mkuu wa ujasusi hadi kuwa mpatanishi wa vita vya Iran

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Rais Trump amsifia Asim Munir kwa utendakazi na kutaja atafika Pakistan hivi karibuni
    • Author, Mariam Mjahid
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Pindi kiongozi mkuu Asim Munir anapoingia katika ukumbi wowote, uzito wa historia ya jeshi ya Pakistan huambatana naye. Hata hivyo, katika miezi ya hivi karibuni, ushawishi wake umevuka mipaka ya kambi za kijeshi za Rawalpindi na kufika hadi Washington, D.C., Tehran na kwingineko duniani.

Munir, ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Pakistan na sasa pia Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Taifa kwa mara ya kwanza, ameibuka kuwa zaidi ya jenerali wa kawaida. Anatajwa kama msuluhishi, mpatanishi na mhimili muhimu wa nguvu za kisiasa, akiwakilisha kurejea kwa ushawishi wa Pakistan katika siasa za kimataifa.

Pakistan iko katika nafasi ya kipekee kwa kuwa inaaminika na Marekani, Iran pamoja na nchi za Ghuba.

Mchakato wa upatanishi unaongozwa na mkuu wa jeshi la Pakistan, Asim Munir, ambaye Rais wa Marekani Donald Trump humtaja kama "kiongozi mkuu wa jeshi'' wake anayempenda zaidi", kwa mujibu wa seneta Mushahid Hussain Syed wa chama tawala cha Pakistan Muslim League.

Munir anachukuliwa kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Pakistan, taifa ambalo kwa muda mrefu jeshi limekuwa na nafasi kuu katika siasa.

Lakini kwanini anazungumziwa sana licha ya kuwa kuna baadhi ya wapatanishi wanaohudhuria vikao Pakistan kupatanisha Marekani na Iran?

Mwanajeshi ageuka kuwa mwanadiplomasia

Jina la Asim Munir limejitokeza zaidi katika mvutano unaoendelea kati ya Iran, Marekani na Israel.

Kwanza kabisa, wakati vita vilivyokuwa vimetanuka dhidi ya Iran na suala la mazungumzo ya amani kuwekwa mezani Assin ameonekana kama nguvu kuu dhidi ya juhudi hizo za kuwaleta pamoja pande hizo mbili.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ni miongoni mwa watu wachache ambao waliwaunganisha viongozi wa Marekani na Iran kupitia mawasiliano ya simu, akipitisha ujumbe kati ya pande hizo mbili kama mpatanishi anayeaminika.

Inaaminika kuwa mazungumzo hayo yanaratibiwa zaidi kutoka Rawalpindi, makao ya jeshi, badala ya Islamabad, ambako ndiko makao ya bunge.

"Field Marshal Munir ndiye nguvu kuu ya mchakato huu, bila yeye isingewezekana," amesema Maleeha Lodhi, aliyewahi kuwa balozi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa, Marekani na Uingereza

Wiki jana esksti rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ametishia kuwa atafuta kizazi kizima cha Iran iwapo hawatakaa mezani, Munir ndiye aliyetuliza roho zao na kuleta muafaka dakika za mwisho na kukubali kufanya mazungumzo ya kusitisha vita.

Na wakati pande hizo mbili zilikutana Islamabad, Amir ndiye alikuwa upande wa tatu, ambapo iliafikiwa kuwa vita visitishwe kwa muda ili kupisha mashambulizi.

Ingawa kulikuwa na vipengele ambavyo Trump alikuwa amemtuma makamu wa rais wa Marekani JD Vance kuzijadili na Iran kikao hicho cha saa 21 hakikufua dafu.

Mlango bahari wa Hormuz uliendelea kufungwa huku Lebanon ikishambuliwa na Israel, jambo lililofanya Iran kusema ahadi za mazungumzo zimekiukwa na kufunga njia hiyo ambayo inavuruga dunia.

Wiki hii Amir aliwasili Iran kama mjumbe na mpatanishi ambapo alipokelewa na Abbas Araqchi ambaye makamu wa Marekani alimtaja kuwa ndiye msingi wa utawala Iran.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alifanya ziara ya kidiplomasia nchini Saudi Arabia kuimarisha uungwaji mkono wa kikanda kwa juhudi za nchi hiyo za kusaka amani.

Trump amekuwa akipendelea kufanya kazi na jeshi la Pakistan badala ya uongozi rasmi wa kidemokrasia uliopo madarani nchini humo.

Maafisa wa Marekani wamemtaja Asim Munir kama "mpatanishi anayeaminika," huku viongozi wa Iran wakikiri juhudi zake za kupunguza mvutano.

Kwa jenerali wa Pakistan kuwa katikati ya mazungumzo ya aina hiyo ni jambo lisilokuwa la kawaida.

Baadhi ya wachambuzi hata walipendekeza jina lake litajwe kwa tuzo ya Nobel Peace Prize. Iwapo atapata heshima hiyo au la, mjadala wenyewe unaonyesha wazi kuongezeka kwa hadhi yake katika jukwaa la kimataifa.

Chanzo cha picha, BBC/ getty

Kuanzia Rawalpindi hadi kilele cha mamlaka

Ni mzaliwa wa mwaka 1968, katika eneo la Rawalpindi huko Pakistan.

Alianza tajiriba yake mwaka 1986 alipopata kamisheni katika Kikosi cha 23 cha Frontier Force.

Kupanda kwake ngazi kulikuwa kwa utaratibu thabiti, lakini wenye mafanikio ya kipekee.

Alipata mafunzo katika Chuo cha Kamandi na afisa cha Pakistan, Chuo Kikuu cha Ulinzi wa Taifa, pamoja na nje ya nchi nchini Japan na Malaysia.

Uzoefu huo ulimjengea mtazamo mpana unaovuka mipaka ya Pakistan, jambo lililokuja kuwa na umuhimu mkubwa baadaye.

Kazi yake ina alama ya upekee, kwani ndiye afisa pekee aliyewahi kuongoza taasisi zote mbili za ujasusi, Ujasusi wa Kijeshi na ujasuasi masuala ya ndani (ISI).

Nafasi hizi zilimweka katikati ya mfumo wa usalama wa Pakistan, na kumpa uelewa wa kina kuhusu uasi wa ndani, ushindani wa kikanda, na mizani nyeti ya mamlaka kati ya taasisi za kiraia na za kijeshi.

Alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi mwezi Novemba 2022, Munir tayari alikuwa amejijengea sifa ya kuwa kiongozi mwenye nidhamu, makini na mwenye mtazamo wa kimkakati.

Hata hivyo, katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, amejituma kama balozi wa kimataifa, akikuza uhusiano wenye nguvu huko Marekani, Saudi Arabiya na Iran.

Kufikia mwisho wa mwaka 2025, alikuwa ametembelea Ikulu ya White House mara mbili, akasimamia mikataba ya Marekani-Pakistani kuhusu uchimbaji madini ya crypto na madini na kutia saini mkataba wa ulinzi na Saudi Arabia.

Hata hivyo, kupaa kwake hakukuishia hapo.

Kuanzia ujasusi hadi Kamanda

Mwezi Desemba 2025, serikali ya Pakistan ilimpandisha cheo Asim Munir na kumpa wadhifa mpya wa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi. Nafasi hii mpya iliunganisha uongozi wa jeshi la nchi kavu, wanamaji na anga, na kumweka chini ya usimamizi wake moja kwa moja.

Wachambuzi walieleza hatua hiyo kuwa ni ya kihistoria katika mabadiliko ya kimkakati ya Pakistan, hasa katika kukabiliana na vita vya kisasa na changamoto za ukanda.

Kwa Munir, hili halikuwa tu kupandishwa cheo, bali lilithibitisha nafasi yake kama mtu mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini humo.

Katika taifa ambalo jeshi limekuwa na nguvu kubwa katika siasa, majukumu yake mapya yalimpa mamlaka makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa.

Asifiwa kimataifa na changamoto nchini Pakistan

Chanzo cha picha, Getty Images

Ukuaji wa hadhi ya Asim Munir katika jukwaa la kimataifa umeirejesha Pakistan kwenye vichwa vya habari kwa sababu zinazovuka migogoro ya kawaida.

Anatazamwa kama mhimili wa utulivu katika eneo lenye misukosuko, kiongozi anayeweza kuzungumza lugha ya nguvu za kijeshi na diplomasia kwa pamoja.

Uwepo wake mjini Washington, D.C. na Tehran unaashiria jitihada za Pakistan kujipambanua upya katika nafasi yake ya kimataifa, si kama dola ya kiusalama pekee bali pia kama mpatanishi.

Hata hivyo, nyumbani changamoto bado zinaendelea.

Pakistan inaendelea kukabiliwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, shinikizo la kiuchumi, na mjadala kuhusu nafasi ya jeshi katika uendeshaji wa serikali.

Wakosoaji wanasema kuimarika kwa mamlaka ya Munir kunaweza kuongeza zaidi ushawishi wa jeshi juu ya taasisi za kiraia, wakati wafuasi wake wakisisitiza kuwa uongozi wake ni muhimu katika kulikabili taifa linalokabiliwa na vitisho vya ndani na nje.

Maisha nje ya utumishi wa kijeshi

Wanajeshi wenzake wamemtaja Asim Munir kuwa ni mtu mwenye nidhamu, mwenye busara katika mawasiliano, na mwenye mkakati wa kina.

Mara chache hutafuta umaarufu miongoni mwa umma, lakini sasa umaarufu huo humuandama.

Mtindo wake wa uongozi ni wa unyenyekevu; hafahamiki kwa hotuba kali au maonesho ya wazi ya kisiasa, bali hujikita katika ushawishi wa kimya, mazungumzo ya makini na hatua zilizopimwa kwa uangalifu.

Umakini huu umekuwa sehemu ya mvuto wake.

Katika zama za siasa zenye kelele nyingi, mtindo wake wa utulivu unaleta tofauti.

Safari yake kutoka mkuu wa ujasusi hadi mpatanishi wa kimataifa inaakisi si tu kupanda kwake binafsi, bali pia jitihada za Pakistan kujipanga upya katika jukwaa la dunia.

Kuganga yajayo

Wakati Asim Munir akiendelea kukabiliana na changamoto za ndani na za kimataifa, hadhi yake inatarajiwa kuendelea kukua.

Iwe ni katika upatanishi kati ya Marekani na Iran, kuimarisha uongozi wa kijeshi nyumbani, au kuongoza mwelekeo wa kimkakati wa Pakistan, sasa yuko katikati ya nyanja mbalimbali za ushawishi.

Swali si kama Munir ana nguvu, bila shaka anazo. Swali ni jinsi atakavyozitumia. Je, ataiongoza Pakistan kuelekea utulivu na nafasi thabiti zaidi kimataifa, au kuimarika kwa mamlaka yake kutaongeza mvutano wa ndani?

Kwa sasa jambo moja liko wazi: Asim Munir si tena kamanda wa vikosi vya kijeshi pekee amekuwa pia kitovu cha ushawishi katika jukwaa la dunia.