Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Afrika inataka ramani mpya ya dunia?
Afrika ndio bara la pili kwa ukubwa duniani likiwa na ukubwa kilomita za mraba millioni 30.37 baada ya bara Asia.
Hata hivyo, kwenye ramani ya Mercator, Afrika huonekana kana kwamba ina ukubwa unaokaribiana na Greenland, eneo ambalo liliwahi kutamaniwa na Donald Trump, ilhali lina chini ya kilomita za mraba milioni 2.5.
Mbali na kuwa jambo la kawaida tu, upotoshaji huu wa ukubwa halisi wa bara la Afrika una athari katika namna watu wanavyoliona bara hili.
Hili ndilo mtazamo wa AU, ambayo inaunga mkono kampeni ya "Correct the map", inayotaka uwakilishi sahihi wa Afrika kwenye ramani.
Ikiwa imepewa jukumu na AU kusaidia kampeni hiyo, Togo sasa itazihimiza mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kutumia ramani inayoonyesha ukubwa halisi wa bara Afrika
Togo inaongoza 'pambano' hilo kwa niaba ya Afrika
Togo inapania kuwahimiza mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuja na ramani ambayo inaelezea ukubwa halisi wa bara Afrika na kutupilia mbali ramani ya Mercator, Waziri wa mambo ya kigeni wa Togo aliliambia shirika la habari la Reuters.
"Ukubwa wa Afrika katika ramani ya dunia si sahihi, na tunataka ukweli wa kisayansi" Alisema Robert Dussey Waziri wa mambo ya kigeni wa Togo.
Mapema mwaka huu, Umoja wa Afrika AU, ilipitisha azimio la kuhimiza uchoraji wa ramani iliyoitwa "Equal Earth Project" na kutaka mataifa wanachama kuachana na Mercator Project.
"Changamoto ya shirika hili ni kuhakikisha azimio hili linakubalia na Umoja wa mataifa na kubadilisha ramani hiyo. Mataifa ya Afrika tayari yanaunga mkono mradi huu."
Dussey anasisitiza kuwa rasimu ya azimio hilo ilikuwa ikiandaliwa na kwamba upigaji kura unapaswa kufanyika katika mkutano mkuu ujao wa Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Septemba 2026.
Umoja wa Afrika AU uliagiza Togo tarehe 7 mwezi Aprili kuwasilisha azimio hilo kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa.
Uwakilishi usio sahihi wa Afrika kwenye ramani
Wakosoaji wanasema kuwa uchoraji wa ramani wa Mercator project, ambao hufanya Greenland ionekane sawa kwa ukubwa na Afrika ilhali kwa kweli Afrika ni takribani mara 14 kubwa zaidi, huimarisha mtazamo wa Afrika kuwa pembezoni licha ya ukubwa wake mkubwa na idadi yake ya watu.
Hali hii pia huathiri mazungumzo yanayoonekana katika vyombo vya habari, elimu na hata katika nyanja za kisiasa.
Ili kurekebisha upotoshaji huu wa Afrika kwenye ramani, Umoja wa Afrika imejiunga na kampeni ya "Correct The Map" inayolenga kusitisha matumizi ya Mercator projection.
Kampeni hii, inayoongozwa na mashirika ya Africa No Filter na Speak Up Africa, inatoa wito wa kupitishwa kwa uchoraji wa ramani wa Equal Earth projection wa mwaka 2018, ambao unalenga kuonyesha ukubwa halisi wa mataifa ya Afrika.
"Uwakilishi sahihi si suala la ramani pekee, unagusa uhuru, maendeleo na nia ya kuhakikisha dunia inaiona Afrika jinsi ilivyo," alisema Moky Makura, mkurugenzi mtendaji wa Africa No Filter, katika mahojiano na Reuters.
Upotoshaji wenye ubaguzi
Upotoshaji unaweza kuwa umeathiri sana mitazamo yetu na kupunguza umuhimu wa bara la Afrika duniani.
Kwa wale wanaotaka kupitishwa kwa ramani mpya, upotoshaji huu wa uhalisia una athari kubwa katika elimu, fikra za pamoja, siasa na vyombo vya habari.
Wanaounga mkono marekebisho ya upotoshaji huu wanaamini kuwa una athari kubwa katika elimu, fikra za pamoja, siasa na vyombo vya habari, na kwamba "kwa watoto wa Afrika, utambulisho wao uko hatarini."
"Huenda ikaonekana kama ni ramani tu ya kawaida, lakini kwa kweli si hivyo," alisema Selma Malika Haddadi, naibu mwenyekiti wa Tume ya umoja wa Afrika, akiongeza kuwa uchoraji wa Mercator projection unatoa hisia ya uongo kwamba Afrika ni "ya pembeni," ilhali kwa kweli ni bara la pili kwa ukubwa duniani kwa eneo, lenye zaidi ya watu bilioni moja. Umoja wa Afrika ina mataifa wanachama 55.
Mercator projection: Ramani ya inayofaa kusahaulika
Ramani ya Mercator projection bado inatumika sana, hasa katika taasisi za elimu na makampuni ya teknolojia kote duniani.
Umoja wa Afrika umeunga mkono kampeni inayolenga kukomesha matumizi ya ramani ya dunia ya karne ya 16 ya Mercator projection, kwa serikali na mashirika ya kimataifa, na badala yake kutumia ramani inayoonyesha kwa usahihi zaidi ukubwa wa Afrika.