Harris hatazungumza usiku wa leo na umati unaondoka
Chanzo cha picha, Holly Honderich / BBC
Takriban dakika 30 zilizopita, uwanja huu katikati mwa Chuo Kikuu cha Howard ulikuwa umejaa wafuasi wa Kamala Harris tayari kusherehekea.
Lakini kwa makadirio kutoka North Carolina na Georgia, ukumbi wa karamu ya usiku wa uchaguzi wa Harris ghafla umesalia mahame.
Mamia ya wafuasi wanatiririka wakiondoka, wengi sasa wanakataa kuzungumza na vyombo vya habari kwani uwezekano wa ushindi wa Harris unaonekana kupotea.
Harris pia hatarajiwi kuzungumza kwenye hafla hiyo
Pendekezo la haki ya uavyaji mimba huko Florida limeshindwa
Chanzo cha picha, Reuters
Pendekezo linalofuatiliwa kwa ukaribu la kurejesha haki za uavyaji mimba huko Florida liko mbioni kushindwa, hili ni pigo kubwa kwa juhudi za kupanua haki ya uavyaji mimba.
Pendekezo hilo lingeruhusu uavyaji mimba wa hadi wiki 24, lakini linapaswa kupata 60% ili kupita.Florida ni mojawapo ya majimbo 10 katika uchaguzi huu ambapo wapiga kura wanaulizwa kuhusu hatua za utoaji mimba.
Hili linakuja baada ya miaka miwili ya Mahakama ya Juu ya Marekani kutoa uamuzi uliofuta haki ya kitaifa ya kutoa mimba, na kusababisha majimbo mengi kuanzisha marufuku au vizuizi vikali dhidi ya uavyaji mimba.
Wanaharakati huko Florida walihimiza marekebisho hayo kama njia ya kupuuza sheria iliyoanza kutumika mapema mwaka huu, ambayo ilipiga marufuku utoaji mimba baada ya wiki ya sita ya ujauzito.
Katika chaguzi zilizopita, mipango ya kupanua haki za utoaji mimba ilipata mafanikio, ikiwa ni pamoja na katika majimbo ya kihafidhina kama vile Kansas.
Uavyaji mimba pia uko kwenye kura katika majimbo kama vile Missouri, Dakota Kusini na Arizona, ambayo yana sheria zinazozuia au kupunguza urahisi wa kuavya mimba.
Tangu uamuzi wa 2022 wa Roe v Wade, majimbo 22 yamebadilisha sheria za utoaji mimba, yakiwemo majimbo 13 ambapo yamepiga marufuku kabisa. Majimbo mengine yameweka vizuizi vya utoaji mimba baada ya wiki sita.
Msimamo wa utawala wa Biden-Harris wa Israel wawaponza huko Michigan
Chanzo cha picha, Getty Images
Dearborn, Michigan, jiji lenye Waarabu wengi, wapiga kura
wote ambao wamezungumza na BBC, walisema wanampigia kura mgombeaji wa Green
Party Jill Stein kwa sababu ya kukatishwa tamaa kwao na msimamo wa Biden-Harris
wa kuunga mkono Israel.
Miongoni mwao ni Sajid Sayed, ambaye alikuwa
akijitambulisha kama mfuasi wa Democrat. Sayed anasema hampendelei Donald Trump
kuliko Kamala Harris, lakini Trump anaweza kuwashawishi baadhi ya wapiga kura
kwasababu alitembelea jamii zao.
Rais huyo wa zamani alikuja Dearborn Ijumaa iliyopita
kukutana na viongozi wa biashara.
"Alisikiliza shida zao," Sayed anasema.
"Alikula chakula cha jioni na wao. Alizungumza na viongozi."
Kufikia sasa hakuna mtu ambaye amesema amempigia kura
Trump - lakini wanafahamu ukweli kwamba kura yao kwa mtu mwingine inaweza kumpendelea
Trump.
"Sijisikii vizuri kuhusu hilo," Sayed anasema.
Lakini, akaongeza, "Ikiwa Harris atashindwa, basi atajua kwamba hiki ndio
chanzo chake."
Upigaji kura wakamilika katika majimbo yote isipokuwa Hawaii na Alaska
Vituo vya kupigia kura katika majimbo yote yamefunga, yakiwemo majimbo ya Pwani ya Magharibi.
Matokeo ya zaidi ya nusu ya majimbo tayari yametangazwa.
Matokeo hayo kufikia sasa yanawiana na kile kilichotarajiwa: Trump ameshinda katika majimbo ya kijadi ya Republican, huku Harris akinyakua ushindi katika ngome za Democratic.
Hakuna hata moja ya majimbo muhimu ambayo yametangazwa kufikia sasa.
Miongoni mwa majimbo ambayo upigaji kura umekamilishwa ni California, ngome ya jadi ya chama cha Democratic ambayo inatarajiwa kumpa Kamala Harris idadi kubwa ya kura 54 ya wawakilishi maalum.
Harris anaungwa mkono na wanawake wengi lakini sio kwa kishindo - kura za maoni
Chanzo cha picha, Reuters
Kumekuwa na mijadala mingi kuhusu mgawanyiko wa kijinsia
katika uchaguzi huu.
Kura za maoni za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wanawake
wanamuunga mkono Harris kwa karibu 54%, ikilinganishwa na 44% kwa Trump.
Lakini Rais Joe Biden alikuwa na mgawanyiko mkubwa wa
kijinsia mnamo 2020, na 57% ya wanawake walimpigia kura.
Data ya kura ya maoni inaongezwa usiku kucha kwa hivyo hii
sio idadi ya mwisho. Pia haifichui kile kinachotokea katika majimbo muhimu ambayo
yeyote anaweza kushinda.
Ukiangalia kinyang’anyiro hicho, Trump anaongoza kwa
wapiga kura wazungu - kundi kubwa zaidi - na Harris anaongoza kwa wapiga kura
weusi.
Pia yuko mbele na wapiga kura wa Kihispania lakini
inaonekana kama uungwaji mkono kwa Trump umeongezeka zaidi ya pointi 10 katika kundi
hili ikilinganishwa na mwaka 2020.
Kura za wawakilishi maalum 270: Je, wagombea hushinda vipi?
Kuna majimbo 50 nchini Marekani na mengi yao hupigia kura
chama kimoja katika kila uchaguzi.
Lakini kuna majimbo machache - yanayojulikana kama
majimbo muhimu - ambapo mgombea yeyote anaweza kushinda.
Majimbo haya ni Nevada, Arizona, North Carolina, Georgia,
Wisconsin, Michigan na Pennsylvania.
Majimbo yenye watu wengi ndio muhimu zaidi, ikitafsiriwa
kwa idadi ya kura 270 za wawakilishi maalum wanaomchagua rais zinazohitajika chini ya mfumo wa kura za
majimbo.
Kuna kura 538 za wawakilishi hao ambazo mgombea anaweza kujinyakulia
kwa jumla.
Rais ajaye atakuwa mgombea atakayepata kura 270
au zaidi za wawakilishi hao maalum.
Wagombea wote wawili watahitajika kushinda angalau
majimbo matatu muhimu ili kuwapitisha kwenye idadi ya kura ambazo ni lazima
kupata.
Trump ashinda katika jimbo la Florida huku shughuli ya kuhesabu kura ikiendelea
Chanzo cha picha, Pool
Shangwe na nderemo zimetawala upande wa Donald Trump huko
Palm Beach, Florida alipotangazwa kuwa anayetarajiwa kupata ushindi katika
jimbo hilo.
Haikuwa na shaka kamwe kwamba angeweza kupata ushindi
katika jimbo hilo ambalo kwa sasa Republican ndio wako kifua mbele.
Kulingana na mchambuzi wa BBC, Anthony Zurcher, siku za jimbo
la Florida kuwa uwanja wa kutafuta ushindi wa urais zimepitwa na wakati.
Miaka 24 iliyopita, kura mia chache katika jimbo hilo zilikuwa
kichocheo cha kupata urais kwa George W Bush wa chama cha Republican dhidi ya
Al Gore wa Democrat.
Kwa sasa, 73% ya kura zikiwa zimehesabiwa, Donald Trump
amekadiriwa kushinda jimbo hilo.
Ni siku nyingine tena tunapokutana katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni 06/11/2024, uchaguzi nchini Marekani unaendelea na tutakufahamisha kila kinachojiri. Karibu.