Britney Spears: Jaji atoa uamuzi wa baba yake Britney kugawana nguvu ya umiliki wa fedha za binti yake

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Britney akifanya maonesho ya tuzo za MTV mwaka 2000

Jaji amekataa ombi la baba yake Britney Spear la kuwa na nguvu zaidi katika udhibiti wa fedha za binti yake.

Jamie Spears amekuwa akidhibiti fedha za mtoto wake tangu mwaka 2008, lakini hivi karibuni mwanamuziki huyo alionesha kuwa anataka baba yake aondolewe.

Alhamisi, jaji aliendeleza uamuzi wa awali wa mahakama kwamba uamuzi wa masuala ya fedha ya mwanamuziki huyo yatafanywa kwa usawa na wote.

Jaji alikataa ombi la Bwana Spears la kuendeleza madaraka ya juu zaidi kama yale ya awali juu ya umiliki wa mali za binti yake.

Uamuzi huo una maanisha kuwa Bwana Spears na kampuni ya kibinafsi ya Bessemer Trust, sasa watakuwa na nguvu sawa ya kudhibiti pesa za mwanamuziki huyo.

Matokeo yake ni kwamba, sasa anatarajiwa kushirikiana na kampuni hiyo kutengeneza bajeti na pendekezo ya uwekezaji wa ujenzi kwa mwanamuzi huyo.

Hatua ya baba yake kuwa na nguvu nyingi katika udhibiti wa fedha za mwanamuziki huyo kulitokana na wasiwasi wa afya ya akili ya mwanamuziki huyo.

Jaji aliyesikiliza kesi hiyo huko Los Angeles, Brenda Penny aliiteua kampuni ya Bessemer Trust kama mshirika mwenza katika udhibiti wa masuala ya fedha ya Britney Spears mnamo mwezi November, lakini akapinga juhudi za mwanamuziki huyo za kutaka kumuondoa kabisa baba yake kama miongoni mwa wanaotoa maamuzi ya kifedha kwa mali zake.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mashabiki wa Britney Spears wanaoendeleza kampeni ya 'Free Britney' nje ya mahakama

Kesi ya Britney Spear na baba yake imengaziwa zaidi na vyombo vya habari hivi karibuni baada ya kurushwa kwa makala iliyoangazia mgogoro wa udhibiti wa mali za mwanamuziki huyo.

Makala hiyo iliyopewa jina la 'Framing Britney Spears', ilitayarishwa na gazeti la New York Times na kuangazia suala hilo kwa undani pamoja na vile mwanamuziki huyo amekuwa akiangaziwa na vyombo vya habari juu ya taaluma yake.

Wakati huo huo, makala hiyo imepelekea kuanzishwa kwa kampeni ya #FreeBritney, na baadhi ya mashabiki wake ambao wanaamini kuwa maisha ya mwanamuziki huyo na taaluma yake yanadhibitiwa kinyume na matakwa yake.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Britney na baba yake Jamie Spears mwaka 2006

Britney Spears hajawahi kufanya maonesho ya moja kwa moja kwa zaidi ya miaka miwili na anasisitiza kuwa hana nia ya kufanya hivyo hadi baba yake atakapoacha kudhibiti taaluma yake.

'Nachukua muda wangu kujifunza kuwa mtu wa kawaida'

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makala inayoangazia udhibiti za fedha za Britney Spears ilitolewa hivi majuzi

Britney Spears alisema kwamba "anachukua muda wake kujifunza kuwa mtu wa kawaida" baada ya makala mpya iliyopeperushwa kuzua gumzo juu ya maisha yake, taaluma yake na afya yake ya akili.

Makala hiyo iliangazia vile alivyoacha kufanya maonesho mwaka 2007, safari ya tiba kwa nyota huyo wa Marekani na mipangilio ya kisheria iliyowekwa.

"Ningependa sana kufanya maonesho," ameandika Britney Spears, 39. "lakini nachukua muda wangu kujifunza kuwa mtu wa kawaida. Nafurahia maisha yangu ya kila siku!"

Aliongeza: "Kila mmoja ana simulizi yake na mitazamo tofauti juu ya maisha ya wengine! Sote tuna maisha tofauti tofauti ya kufurahisha.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Britney Spears

Wakati huo huo mchumba wake Britney Spears Sam Asghari, amemkosoa baba yake Britney kwenye mitandao ya kijamii.

"Ni muhimu kwa watu kuelewa kuwa sina heshima kabisa kwa mtu ambaye anajaribu kudhibiti uhusiano wetu na kila wakati anakuwa kizuizi maishani mwetu," aliandika hivyo kwenye ujumbe alioandika katika mtandao wa Instagram.

Hali ya fedha za Britney kudhibitiwa imefikaje hapo?

Hali hii huwa ni maamuzi yanayofanywa na mahakama dhidi ya watu ambao hawawezi kujifanyia maamuzi yao wenyewe, iwapo watawekwa katika kundi la wenye ugonjwa wa akili wa dementia au matatizo mengine ya akili.

Chini ya makubaliano ya kisheria, Spears hajakuwa akidhibiti fedha zake au taaluma yake tangu uamuzi huo ulipotolewa mwaka 2008.

Badala yake, baba yake na mawakili wake wamekuwa na nguvu ya kumfanyia maamuzi kuhusu maisha yake ya kibinafsi.

Pia matumizi yake ya kifedha ni lazima yarekodiwe mahakamani.

Hadi kufikia mwaka 2018, inasemekana Spears alikuwa na utajiri wa dola milioni 59 kulingana na tovuti ya masuala ya fedha ya Marekani, Business Insider.

Mwaka huo huo, Spears alitumia dola milioni 1.1 kama ada ya kisheria, kulingana na nyaraka za mahakama zilizoangaziwa na tovuti ya Entertainment Tonight.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Justin Timberlake na Britney Spears walikuwa wanandoa ambao vyombo vya habari vilipenda kuwaangazia kabla ya kuachana mwaka 2002

Kwanini Britney aliwekewa zuio la kujidhibiti kifedha?

Spears alianza kuonesha tabia zisizoeleweka mwaka 2007 baada ya kutalakiana rasmi na aliyekuwa mume wake Kevin Federline na akapoteza haki ya kutunza watoto wake wawili.

Madai ya kuwa na matatizo ya akili yalijitokeza hadharani - aligonga vichwa vya habari kwa kunyoa nywele zake na pia aligonga vichwa vya habari alipopiga gari la aliowashuku kuwa wanahabari wadaku kwa mwavuli, baada ya kubaini kwamba wanataka kumpiga picha.

Aidha, alipata huduma kituo cha kurekebisha tabia mara kadhaa.

Pia alianza kupewa matibabu ya afya ya akili baada ya kukataa kuachia vijana wake katika mgogoro na polisi na hali ya kudhibitiwa kifedha dhidi yake ikaanza kutekelezwa mapema mwaka 2008.

Lakini hata wakati anadhibitiwa kifedha, Spears amekuwa akiendeleza shughuli zake: alitoa albamu tatu na kujitokeza katika vipindi vya televisheni mara kadhaa.