Papa alivyowakosoa vikali wageni wanaoitumia vibaya Afrika kwa ajili ya faida yao

    • Author, Lucy Fleming
    • Author, Paul Njie
    • Nafasi, BBC Africa
    • Akiripoti kutoka, Bamenda
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Papa Leo XIV amewakosoa wageni wanaoitumia vibaya rasilimali za Afrika kwa ajili ya faida wakati wa ziara yake katika eneo la Cameroon lililoathiriwa na migogoro.

Hii ni mojawapo ya kauli kadhaa za moja kwa moja alizotoa katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kukosoa wale wanaotumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya vita na kuiambia serikali ya Cameroon kushughulikia ufisadi ili amani iweze kupatikana.

Ametumia siku nzima katika mji wa Bamenda, ambao uko katikati ya uasi mkali na wa muda mrefu wa wanaojitenga nchini Cameroon.

Alisema matatizo ya ndani yamechochewa zaidi na watu wa nje ambao "kwa faida yao, wanaendelea kuingilia na kuitumia vibaya bara la Afrika ili kulinyonya na kulipora," alihutubia takriban waumini 20,000 katika Misa iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Bamenda.

Mapema, umati wa watu wenye furaha waliimba, walipiga ngoma na kupeperusha bendera kumkaribisha kiongozi wa Kanisa Katoliki, ambaye aliwasili chini ya ulinzi wa kijeshi akiwa kwenye gari jeupe lisilopenya risasi.

Kabla ya ziara yake, wanaojitenga wanaozungumza kiingereza walikuwa wametangaza kipindi cha "njia salama ya usafiri."

Kituo cha kwanza cha Papa kilikuwa katika mkutano wa amani uliofanyika Bamenda katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, ukihusu uasi wa karibu miaka 10 katika maeneo mawili ya Cameroon yanayozungumza Kiingereza, ambao umesababisha vifo vya takribani watu 6,000 na kuwafanya wengine wengi kukimbia makazi yao.

"Dunia inaharibiwa na kundi dogo la madikteta," kauli zinazokuja kufuatia ukosoaji wa hivi karibuni wa Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya Papa huyo, ambaye mwaka jana alikua Papa wa kwanza mzaliwa wa Marekani.

"Wale wanaopora rasilimali za ardhi yenu kwa kawaida huwekeza sehemu kubwa ya faida katika silaha, hivyo kuendeleza mzunguko usio na mwisho wa machafuko na vifo," alisema Papa huyo mwenye umri wa miaka 70.

Tangu mwaka 2017, wanaotaka kuunda taifa jipya katika eneo la Anglophone la Cameroon wamekuwa wakipigana na majeshi ya serikali.

Wamekasirishwa na kile wanachokiona kama kutengwa na kunyimwa haki kwa wachache wanaozungumza Kiingereza na serikali inayotawaliwa na wanaozungumza Kifaransa.

Viongozi wa dini na waathirika wa mgogoro wa Anglophone kwa zamu walieleza athari za mapigano hayo kwa Papa.

Kiongozi mmoja wa Kiislamu alilalamikia mauaji ya wanajamii wa asili wa Mbororo, pamoja na uporaji wa ng'ombe na mali nyingine.

Mtawa mmoja wa kike alifichua maelezo ya kutekwa nyara kwake na wapiganaji wanaotaka kujitenga, akionesha ukali wa mgogoro huo.

Mwanaume mwingine alieleza jinsi alivyolazimika kukimbia nyumbani kwake.

Papa aliwasifu kwa kazi yao na kusema ni mfano kwa dunia nzima: "Tumshukuru Mungu kwamba mgogoro huu haujageuka kuwa vita vya kidini."

Wachambuzi wanasema Papa amekuwa mkweli sana katika hotuba zake nchini Cameroon.

Siku ya Jumatano katika ikulu ya rais katika mji mkuu, Yaoundé, alitoa ushauri mkali kwa serikali wakati wa hotuba iliyohudhuriwa pia na Rais Paul Biya.

"ili amani na haki vitawale, minyororo ya ufisadi, ambayo huharibu mamlaka na kuondoa uaminifu wake,lazima ivunjwe," alisema.

Rais wa Cameroon mwenye umri wa miaka 93, Paul Biya, alishinda muhula wa nane mwaka jana katika uchaguzi uliozozaniwa, na serikali yake inakosolewa kwa madai ya ufisadi, uongozi mbaya na kushindwa kushughulikia masuala ya usalama.

"Mioyo lazima iachwe huru kutoka katika tamaa ya kipumbavu ya kujipatia faida," alisema Papa, huku kiongozi huyo mkongwe zaidi duniani akibaki bila kuonesha hisia zozote.

Televisheni ya taifa ilisitisha matangazo ya moja kwa moja kwa sehemu ya hotuba ya Papa, kulingana na Associated Press, ambayo ilisema haijulikani kama kulikuwa na matatizo ya kiufundi.

Katika hotuba hiyo hiyo, Papa pia aliwataja vijana kama tumaini la Cameroon na Kanisa.

"Nguvu zao na ubunifu wao ni wa thamani kubwa. Kuwekeza katika elimu yao, mafunzo na ujasiriamali ni muhimu kwa amani na kuzuia kupotea kwa vipaji na kuenea kwa matatizo ya kijamii," alisema.

"Ningependa pia kuangazia nafasi ya wanawake, ambao mara nyingi huwa waathirika wa dhuluma, lakini ni wajenzi wasiochoka wa amani. Sauti yao lazima itambuliwe kikamilifu katika maamuzi."

Biya alikuwa ameahidi kuwapa kipaumbele wanawake na vijana baada ya kushinda uchaguzi tena mwezi Oktoba, huku matarajio yakiwa makubwa wakati mabadiliko ya baraza la mawaziri yakitarajiwa.

Askofu Mkuu wa Bamenda, Andrew Nkea, amesema ziara ya Papa italeta matumaini kwa watu ambao maisha yao yamevurugwa na mgogoro katika maeneo ya Kaskazini-Magharibi na Kusini-Magharibi mwa Cameroon.

"Ninaweza kusema kwa uhakika sasa ni wakati wa amani," alisema Nkea.

Maneno haya yalisisitizwa pia na Papa katika Misa iliyofanyika baadaye uwanjani, ambapo gari lake lilizunguka uwanja wa ndege mara kadhaa ili kuwasalimia umati uliokuwa ukishangilia huku kwaya zikiimba.

Alisema mabadiliko yanawezekana ikiwa watu watamtii Mungu, si wanadamu.

"Wakati umefika, leo na si kesho, sasa na si baadaye, kurejesha umoja kwa kuunganisha utofauti na utajiri wa nchi na bara.

"Tunapaswa kumtii Mungu badala ya mamlaka yoyote ya kibinadamu."

Amani ndiyo mada kuu ya ziara ya Papa ya siku 11 barani Afrika, huku Angola na Guinea ya Ikweta zikiwa hatua zinazofuata katika ratiba yake.

Alianza ziara yake nchini Algeria siku ya Jumatatu, ikiwa ni ziara ya kwanza kwa Papa yeyote katika nchi hiyo yenye Waislamu wengi.

Pia ni mahali alipozaliwa Augustine of Hippo, ambaye alianzisha shirika la kidini linalofuatwa na Papa Leo, akiwa Papa wa kwanza kufanya hivyo.

Katika siku zake mbili nchini Algeria, alitembelea Msikiti Mkuu wa Algiers.

"Naamini ziara ya msikitini ilikuwa muhimu kuonesha kwamba ingawa tuna imani tofauti, njia tofauti za kuabudu na kuishi, tunaweza kuishi pamoja kwa amani," alisema baada ya hapo.