Pendekezo linalofuatiliwa kwa ukaribu la kurejesha haki za uavyaji mimba huko Florida liko mbioni kushindwa, hili ni pigo kubwa kwa juhudi za kupanua haki ya uavyaji mimba.
Pendekezo hilo lingeruhusu uavyaji mimba wa hadi wiki 24, lakini linapaswa kupata 60% ili kupita.Florida ni mojawapo ya majimbo 10 katika uchaguzi huu ambapo wapiga kura wanaulizwa kuhusu hatua za utoaji mimba.
Hili linakuja baada ya miaka miwili ya Mahakama ya Juu ya Marekani kutoa uamuzi uliofuta haki ya kitaifa ya kutoa mimba, na kusababisha majimbo mengi kuanzisha marufuku au vizuizi vikali dhidi ya uavyaji mimba.
Wanaharakati huko Florida walihimiza marekebisho hayo kama njia ya kupuuza sheria iliyoanza kutumika mapema mwaka huu, ambayo ilipiga marufuku utoaji mimba baada ya wiki ya sita ya ujauzito.
Katika chaguzi zilizopita, mipango ya kupanua haki za utoaji mimba ilipata mafanikio, ikiwa ni pamoja na katika majimbo ya kihafidhina kama vile Kansas.
Uavyaji mimba pia uko kwenye kura katika majimbo kama vile Missouri, Dakota Kusini na Arizona, ambayo yana sheria zinazozuia au kupunguza urahisi wa kuavya mimba.
Tangu uamuzi wa 2022 wa Roe v Wade, majimbo 22 yamebadilisha sheria za utoaji mimba, yakiwemo majimbo 13 ambapo yamepiga marufuku kabisa. Majimbo mengine yameweka vizuizi vya utoaji mimba baada ya wiki sita.