Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran: Tutashambulia "Ukanda wa Gaza"
Jeshi la Iran IRGC limesema katika taarifa kwamba Israel "imevuka mipaka yote myekundu katika mauaji ya halaiki na kuendelea kwa mchakato huu sio jambo la kustahimili."
Muhtasari
- Qatar: Hatutapatanisha Iran na Marekani
- Mwanadiplomasia wa Iran ataja nchi itakayoshughulikia mazungumzo ya kusitisha mapigano
- Iran: Tutashambulia "Ukanda wa Gaza"
- Lebanon yabatilisha hati za uwakilishi za balozi wa Iran
- Iran yamimina makombora ndani ya Israel na kukejeli mazungumzo ya Trump ya kudhibiti kwa pamoja eneo la bahari
- Umoja wa Ulaya waeleza kuwa na "wasiwasi mkubwa" kuhusu vita vya Mashariki ya Kati
- Katika Picha: Hali ilivyo nchini Israel kufuatia shambulizi la Iran
- Israel yathibitisha kupata maafa makubwa kufuatia mashambulizi ya Iran
- Rais wa Marekani Donald Trump atuma ujumbe Iran
- Marekani yasema mipango ya mazungumzo ya Iran bado ni 'tete'
- Watoto 208 wauawa Iran kwa mashambulizi ya Marekani na Israel
- Waziri wa Israel asema wanajeshi wakalie eneo la kusini mwa Lebanon
- Watu wakamatwa Nigeria baada ya video kusambaa mtandaoni za unyanyasaji wa kingono katika tamasha
- Waziri wa zamani wa mambo ya nje Kenya akamatwa kwa kupanga kutoweka kwake
- Ndege ya jeshi yaanguka Colombia na kuua watu 66
- Trump aipa Iran 'nafasi ya mwisho' ya mazungumzo ya amani
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Mariam Mjahid
Shirika la ndege la Kenya Airways latangaza hasara ya dola milioni 138
Peter Mwangangi
Mwandishi BBC
Shirika la ndege la Kenya Airways (KQ) limetangaza hasara ya kabla ya kodi ya dola milioni 138.30 (sawa na shilingi bilioni 17.93 za Kenya) kwa mwaka 2025.
Hali hii inajiri mwaka mmoja tu baada ya shirika hilo kurekodi faida ya dola milioni 41.7, ikiwa ni faida yake ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Faida hiyo ya mwaka 2024 ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarika kwa thamani ya sarafu ya Kenya dhidi ya dola ya Marekani.
Kwa mujibu wa shirika hilo, licha ya kuendelea kuwepo kwa mahitaji ya usafiri wa anga, changamoto kuu imekuwa upungufu wa ndege za kutoa huduma. Ndege zake tatu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner zimeshindwa kufanya safari kutokana na uhaba wa vipuri katika soko la kimataifa.
Katika juhudi za kuboresha hali hiyo, KQ inapanga kuongeza ndege moja katika safari zake kuelekea Uwanja wa Ndege wa Heathrow Airport, jijini London, kuanzia mwezi Julai 2026, sambamba na mikakati mingine ya kufufua utendaji wake.
Aidha, uongozi wa shirika hilo unabainisha kuwa vita vinavyoendelea katika Mashariki ya Kati vimeongeza mahitaji ya viti vya usafiri, hususan kutoka bara Ulaya, Asia na Marekani.
Mnamo Desemba 2025, KQ ilitangaza mabadiliko ya uongozi ambapo Afisa Mkuu Mtendaji, Allan Kilavuka, aliondoka baada ya kulitumikia shirika hilo kwa miaka sita, huku Kapteni George Kamal akiteuliwa kukaimu nafasi hiyo.
Soma zaidi:
Starlink ya Elon Musk yapigwa marufuku kuendesha biashara Namibia
Namibia imekataa maombi ya kampuni ya Elon Musk inayomiliki Starlink ya kupata leseni ya kutoa huduma za intaneti kupitia satelaiti nchini humo, ikimpa kampuni hiyo kizuizi cha pili katika Afrika Kusini.
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano ya Namibia (Cran) ilitangaza uamuzi huo bila kutoa sababu za kukataa, lakini ikabainisha kuwa tawi la Starlink nchini Namibia halina umiliki wa wenyeji.
Starlink bado haijatoa maoni yoyote kuhusu uamuzi huo.
Kampuni hiyo inaendesha huduma katika takriban nchi 25 za Afrika lakini imekabiliana na changamoto za udhibiti katika nchi nyingine, ikiwemo Afrika Kusini, ambapo sheria za umiliki pia zimezuia kuingia kwake.
Sheria za Namibia zinahitaji angalau hisa 51% katika kampuni yoyote ya mawasiliano ziwe zikiwa katika umiliki wa raia au mashirika ya ndani.
Namibia ni koloni la zamani la Ujerumani, na ilikuwa chini ya utawala wa wazungu wa Afrika Kusini hadi ilipopata uhuru mwaka 1990.
Baada ya uhuru, nchi hiyo ilianzisha sera zinazolenga kuongeza umiliki wa ndani katika biashara na kushughulikia ukosefu wa usawa wa rangi.
Kwenye tovuti yake, Starlink imesema imeanzisha kampuni ya ndani itakayoshirikiana na kampuni za Namibian na kuunda fursa za ajira.
Cran ilisema inaweza kuzingatia tena uamuzi wake ama “kwa hiari yake mwenyewe au kutokana na rufaa ya upande ulioathirika” ndani ya siku 90.
Mnamo 2024, mratibu huyo aliagiza Starlink, akidaiwa kuendesha shughuli bila leseni na kuiagiza kampuni hiyo kusitisha mara moja operesheni zake zote Namibia.
Pia aliwaonya wananchi kuto nunua vifaa vya Starlink au kujiandikisha kwa huduma zake, kwani kufanya hivyo ingekuwa kinyume cha sheria.
Musk, aliyezaliwa Afrika Kusini mwaka 1971 kabla ya kuhamia Canada mwishoni mwa miaka ya 1980 na kisha Marekani ambapo akawa mtu tajiri zaidi duniani, amelaumu “sheria za umiliki zenye ubaguzi wa rangi” kwa kushindwa kwa kampuni yake kuanzisha huduma Afrika Kusini.
Katika chapisho alilolitoa mwaka jana kwenye mtandao wa X, alidai kuwa mtoa huduma yake ya intaneti kupitia satelaiti “hakupewa ruhusa kuhudumu Afrika Kusini kwa sababu mimi si mtu mweusi.”
Pia ilibainisha kuwa zaidi ya kampuni 600 za Marekani, ikiwemo kampuni kubwa ya kompyuta Microsoft, zinaendesha shughuli Afrika Kusini kwa kuzingatia sheria zake na “zinafanikiwa.”
Sera za uwezeshaji wa watu weusi zilianzishwa baada ya utawala wa wazungu walio wachache kuisha 1994, kwa lengo la kushughulikia ubaguzi wa rangi wa zamani.
Hii imejumuisha kuanzisha sheria zinazohitaji wawekezaji kutoa hisa 30% kwa kampuni za waafrika wa ndani katika biashara Afrika Kusini.
Starlink inatoa huduma za intaneti kupitia mtandao mkubwa wa satelaiti. Huduma yake inalenga watu wanaoishi katika maeneo ya mbali ambao hawawezi kupata intaneti ya kasi ya juu.
Soma zaidi:
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akataa kusitisha mashambulizi dhidi ya Iran
Licha ya migongano katika malengo ya Marekani, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amefafanua wazi kuwa nchi yake itaendelea kushambulia Iran na mshirika wake, Hezbollah, kusini mwa Lebanon.
Katika ujumbe mfupi wa video, alionya:“Tutalinda maslahi yetu kwa gharama yoyote.”
Iran bado ina uwezo wa kulipiza kisasi dhidi ya Israel, huku shambulio lake la hivi karibuni la makombora lilisababisha shimo kubwa katika eneo la makazi mjini Tel Aviv.
Maafisa wanasema shambulio hilo lilitumia takriban kilo 100 za vilipuzi.
“Kwa sasa ninaona bango karibu nami lenye picha ya Donald Trump akiwa na bendera ya Marekani na maneno: ‘Bwana Rais, fanya hili ulifanikishe.’”
Inaonekana kuwa Israel haina mpango wa kumaliza mzozo huu hivi karibuni.
Soma Pia:
Wairani wanaambiwa nini kuhusu vita
Iran yamteua mkuu mpya wa baraza la usalama la Iran baada ya kuuawa kwa Larijani
Vyombo vya habari vya Iran vinaripoti kuwa Mohammad Bagher Zolghar ameapishwa kuwa katibu wa Baraza la kitaifa la Usalama, kwa mujibu wa afisa mmoja katika ofisi ya urais ya Iran.
Uteuzi huu unafuata mauaji ya afisa mkuu wa zamani wa usalama, Ali Larijani, tarehe 17 Machi.
Zolghar ameshika nafasi nyingi za juu, ikiwemo naibu kamanda wa IRGC, naibu waziri wa ndani wa masuala ya usalama, naibu mkuu wa tume ya sheria, na katibu wa baraza lenye nguvu.
Soma pia:
Ubalozi wa Marekani ulioko Muscat umeondoa agizo la kukaa sehemu salama kwa raia wake
Ubalozi wa Marekani mjini Muscat umeondoa sharti la kukaa kwa kujihifadhi kwa raia wake katika mji mkuu wa Oman.
Ushauri wa kujikinga ulikuwa umetolewa saa 20:42 saa za ndani (16:42 GMT).
Wizara inasema kwamba wakati ushauri huu umeondolewa kwa mji mkuu, "makazi katika mwongozo yanasalia kwa Oman nzima kutokana na shughuli inayoendelea".
Ubalozi unawaambia raia: "Kwa kadiri inavyowezekana, baki katika makazi yako, hoteli, au hifadhi nyingine, na kaa mbali na madirisha."
Pia unaweza kusoma:
Qatar: Hatutapatanisha Iran na Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar amesema Doha haihusiki na juhudi zozote za Marekani na Iran za kumaliza vita hivyo.
Majid Ansari alisema: "Lengo letu ni kukomesha mashambulizi dhidi ya nchi yetu na kulinda nchi yetu."
Katika miaka ya nyuma, haswa kabla ya vita vya siku 12, Qatar ilikuwa mmoja wa wapatanishi wakuu kati ya Iran na Marekani.
Katika kujibu swali la iwapo Qatar inaweza kuwa na uhusiano wa kawaida na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya mashambulizi ya Iran katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, Bw Ansari alijibu: "Ndiyo, hatuwezi kubadilisha jiografia."
Mwanadiplomasia wa Iran ataja nchi itakayoshughulikia mazungumzo ya kusitisha mapigano
Mwanadiplomasia wa Iran anayefahamu uwezekano wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani ameiambia BBC News Urdu kuwa kuna “uwezekano mdogo wa mazungumzo hayo.”
“Ikiwa uamuzi wa mwisho utafikiwa (kuhusu mazungumzo hayo), Islamabad inaweza kuwa moja ya maeneo ya kuyafanyia majadiliano,” alisema, kwa sharti la kutotajwa jina.
“Tunangoja maelezo kutoka Wizara yetu ya Mambo ya Nje.”
Inafaa kutajwa kuwa Jumapili, Rais wa Marekani alidai kuwa Marekani na Iran zimekuwa na “mazungumzo mazuri, yenye tija na yenye kujenga” ya kupunguza mvutano.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilikanusha kuwepo kwa mazungumzo yoyote kati ya Tehran na Washington.
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alizungumza kwa simu na Rais wa Iran, Masoud Peshmerga, Jumatatu na kutoa wito wa “kupunguza mvutano mara moja na kutatua tofauti kupitia mazungumzo na diplomasia na nchi jirani.”
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Shehbaz Sharif alihakikishia uongozi wa Iran kuwa “Pakistan itaendelea kuchukua nafasi ya kujenga katika kuleta amani katika ukanda huo.”
Pia unaweza kusoma:
Habari za hivi punde, Iran: Tutashambulia "Ukanda wa Gaza"
Walinzi wa Mapinduzi ya jeshi la Iran IRGC wamesema katika taarifa kwamba Israel "imevuka mipaka yote mekundu katika mauaji ya halaiki na kuendelea kwa mchakato huu sio jambo la kustahimili."
Katika taarifa hii, IRGC "imelitahadharisha" jeshi la Israel kwamba "kama uhalifu dhidi ya raia wa Lebanon na Palestina utaendelea, maeneo ya mikusanyiko ya maadui kaskazini mwa Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Ukanda wa Gaza yatakabiliwa na mashambulio mazito ya makombora na ndege zisizo na rubani bila kuzingatia chochote."
Lebanon yabatilisha hati za uwakilishi za balozi wa Iran
Abdel Sattar Issa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon, amemuita Tawfiq Samadi Khoshkho, Balozi wa Iran mjini Beirut, na kumfahamisha kuhusu kufutwa kwa hati za utambulisho za Mohammad Reza Rauf Sheibani, balozi wa Iran.
Amechukuliwa kuwa "kipengele kisichohitajika" na ameombwa kuondoka Lebanon hadi Jumapili ijayo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon pia ilimuita balozi wake Ahmed Suwaidan kutoka Tehran kwa mashauriano.
Uhusiano wa serikali ya Lebanon na serikali ya Iran unazidi kuzorota.
Hezbollah ni mshirika wa karibu wa Iran, na serikali ya Lebanon iko chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa Marekani na Israel kuwapokonya silaha Hezbollah.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon Youssef Raji alisema mwaka jana kwamba alikataa mwaliko wa kusafiri kwenda Tehran na badala yake akapendekeza mazungumzo hayo yafanyike katika nchi ya "tatu na isiyoegemea upande wowote" iliyokubaliwa na pande zote mbili.
Soma zaidi:
Iran yamimina makombora ndani ya Israel na kukejeli mazungumzo ya Trump ya kudhibiti kwa pamoja eneo la bahari
Iran yarusha makombora kuelekea Israel Jumanne, jeshi la Israel lilisema, siku moja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kusema kulikuwa na mazungumzo “mazuri sana na yenye tija” yaliyolenga kusitisha mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.
Maafisa watatu waandamizi wa Israel, waliokubali kuzungumza bila kutajwa majina, wamesema Trump anaonekana kuwa na azma ya kufikia makubaliano, lakini wanaona kuwa ni vigumu sana kwa Iran kukubali masharti ya Marekani katika duru yoyote mpya ya mazungumzo.
Baada ya kauli ya Trump kupitia Truth Social Jumatatu, Iran ilisema kuwa hakuna mazungumzo yaliyofanyika hadi sasa.
Ubalozi wa Iran nchini Afrika Kusini ulichapisha picha kwenye mtandao wa X ikionyesha usukani mdogo wa waridi wa mtoto uliowekwa kwenye dashibodi ya gari mbele ya kiti cha abiria, hatua iliyotafsiriwa kama kejeli kwa wazo la Trump, alilolitoa kwa waandishi wa habari, kwamba angeweza kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz pamoja na kiongozi mkuu wa Iran.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye alizungumza na Trump chini ya saa 48 kabla ya nchi zao kuanza vita, alitarajiwa kuitisha mkutano wa maafisa wa usalama kujadili juhudi za Trump za kufikia makubaliano na Iran, kwa mujibu wa maafisa wawili waandamizi wa Israel.
Afisa mmoja wa Pakistan amesema mazungumzo ya moja kwa moja yanaweza kufanyika mjini Islamabad wiki hii.
Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi dhidi ya Iran tarehe 28 Februari baada ya kusema hazijapata mafanikio ya kutosha katika mazungumzo yaliyolenga kusitisha mpango wa nyuklia wa Iran, licha ya mpatanishi Oman kusema kulikuwa na maendeleo makubwa.
Mgogoro huo umeongezeka kote Mashariki ya Kati.
Iran imeshambulia nchi zinazohifadhi vituo vya kijeshi vya Marekani, imelenga miundombinu muhimu ya nishati na kwa kiasi kikubwa imefunga Mlango-Bahari wa Hormuz, njia inayopitisha takribani theluthi moja ya tano ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani.
Soma Pia:
Umoja wa Ulaya waeleza kuwa na “wasiwasi mkubwa” kuhusu vita vya Mashariki ya Kati
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ameeleza “wasiwasi mkubwa” kuhusu migogoro inayoendelea katika Mashariki ya Kati, na kusisitiza umuhimu wa kufikiwa kwa amani kupitia mazungumzo ili kumaliza vita vya Iran.
“Ni muhimu sana tupate suluhisho la mazungumzo ambalo litakomesha migogoro tunayoishuhudia katika Mashariki ya Kati,” alisema akiwa mjini Canberra pamoja na Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese.
Bi. von der Leyen pia alitangaza kuwa baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zinajiandaa kushiriki katika “operesheni” ya kulinda Mlango-Bahari wa Strait of Hormuz baada ya kumalizika kwa vita.
Aliongeza: “Sote tunahisi athari zisizo za moja kwa moja za mgogoro huu katika bei za gesi na mafuta, biashara zetu na jamii zetu,” akisisitiza kuwa njia hii ya biashara (mkono-bahari wa Hormuz) ni “muhimu sana kwa usambazaji wa nishati kwa washirika duniani kote.”
Soma pia:
Katika Picha: Hali ilivyo nchini Israel kufuatia shambulizi la Iran
Hapo awali tuliripoti kwamba timu za utafutaji na uokoaji zilitumwa hadi Israeli ya kati baada ya kugonga roketi.
Sasa picha kutoka Tel Aviv zimesambazwa mitandaoni.
Picha hizi zinaonyesha moshi ukifuka katika baadhi ya maeneo ya jiji na vikosi vya uokoaji vinavyofanya kazi katika eneo la mashambulizi.
Sehemu ya jengo pia imeporomoka.
Kiwango kamili cha uharibifu bado hakijajulikana.
Israel yathibitisha kupata maafa makubwa kufuatia mashambulizi ya Iran
Jeshi la Israel limethibitisha kuwa shambulio la makombora kutoka Iran limesababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya kati ya nchi, huku vikosi vya dharura na wahudumu wa misaada wakitumwa haraka katika maeneo yaliyoathirika.
Picha zilizochapishwa kupitia ukurasa wa Telegram wa huduma za dharura za Israel zinaonesha moshi mzito ukifuka kutoka kwenye majengo, pamoja na vifusi vilivyotapakaa katika eneo lilolengwa na shambulio hilo.
Awali, iliripotiwa kuwa kufuatia tahadhari iliyotolewa na jeshi la Israel kuhusu makombora yaliyofyatuliwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC), wahudumu wa misaada walielekezwa kusini mwa nchi, ambako kulishuhudiwa uharibifu mkubwa kufuatia mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel.
Katika siku za karibuni, picha zimekuwa zikisambaa zikionesha kiwango kikubwa cha uharibifu nchini Israel.
Soma zaidi:
Rais wa Marekani Donald Trump atuma ujumbe Iran
Marekani imetuma ujumbe kwa Iran kupitia mjumbe maalum, na ujumbe huo uliwasilishwa kwa Iran, kwa mujibu wa shirika la habari la Marekani, CBS News, likinukuu afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Trump alitangaza jana kuwa alikuwa amefanya mazungumzo na Iran kwa muda wa siku mbili, na kwamba mazungumzo hayo yataendelea wiki hii.
Baada ya kauli ya Trump, Iran ilikanusha kuwepo kwa mazungumzo yoyote na Marekani.
Hata hivyo, baadaye Iran ilithibitisha kuwa ujumbe kutoka Marekani uliwasilishwa kupitia nchi nyingine, kama ilivyoripotiwa na CBS News.
“Tumeupokea ujumbe kutoka Marekani. Kwa sasa unafanyiwa tathmini,” alisema afisa mmoja wa Iran, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.
Trump alisema katika taarifa yake jana kuwa alikuwa amefanya mazungumzo yenye tija na Iran na kuwasilisha hoja 15.
“Iran inataka amani; ninaamini kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa makubaliano,” Trump aliwaambia waandishi wa habari.
Marekani na Iran hazina uhusiano wa moja kwa moja wa kidiplomasia.
Badala yake, zimekuwa zikiwasiliana na kufanya mazungumzo kupitia nchi nyingine.
Soma zaidi:
Marekani yasema mipango ya mazungumzo ya Iran bado ni 'tete'
Ikulu ya White House siku ya Jumatatu ilionekana kukabilia uvumi kuhusu uwezekano wa mazungumzo kati ya Marekani na Iran juu ya vita vinavyoendelea baada ya Rais Donald Trump kupendekeza pande hizo mbili zinafanya maendeleo "makubwa" kuelekea makubaliano.
Maoni ya Trump kuhusu mazungumzo yalisababisha ripoti kwamba Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance anaweza kuiwakilisha serikali katika mazungumzo kati ya Marekani na Iran nchini Pakistan.
Lakini Ikulu ya Marekani inasema hali ni "mbaya" na ikaonya kwamba hakuna mikutano rasmi kati ya viongozi wakuu kutoka Marekani na Iran iliyotangazwa.
"Hizi ni mijadala nyeti ya kidiplomasia na Marekani haitajadiliana kupitia vyombo vya habari," Karoline Leavitt, katibu wa habari wa Ikulu ya White House, aliambia BBC katika taarifa.
"Hili ni jambo tete, na uvumi kuhusu mikutano haupaswi kuchukuliwa kama hatua ya mwisho hadi itakapotangazwa rasmi na Ikulu ya White House," Leavitt anasema.
Soma zaidi:
Watoto 208 wauawa Iran kwa mashambulizi ya Marekani na Israel
Mkuu wa huduma za dharura anasema idadi ya watoto waliouawa nchini Iran tangu vita kuanza Februari 28 imeongezeka hadi 208.
Katika taarifa ya video iliyochapishwa na mtangazaji wa kituo kinachomilikiwa na serikali IRIB, Jafar Miadfar alisema kwamba kati ya watoto 208 waliouawa, sababu ya 168 kufariki dunia kati ya hao ilikuwa ni mashambulizi la makombora ya Marekani kwenye shule ya wasichana katika mji wa Minab mwanzoni mwa vita.
Miadfar aliongeza kuwa watoto 13 waliouawa walikuwa na umri chini ya miaka mitano, na mdogo alikuwa na siku tatu.
Zaidi ya raia 1,500 wameuawa kote nchini hadi sasa, kulingana na serikali ya Iran.
Video zilizothibitishwa na picha za setilaiti zilionyesha uharibifu mkubwa karibu na shule ya msingi ya Shajareh Tayebeh huko Minab na eneo la karibu la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Irani (IRGC).
Pia inaonyesha kuwa eneo hilo "lilishambuliwa vibaya wakati mmoja au karibu wakati mmoja", alisema mtaalamu wa silaha NR Jenzen Jones.
Pia unaweza kutazama:
Waziri wa Israel asema wanajeshi wakalie eneo la kusini mwa Lebanon
Waziri wa fedha wa Israel amesema siku ya Jumatatu kuwa Israel inapaswa kupanua mpaka wake na Lebanon hadi Mto Litani ndani kabisa ya kusini mwa nchi hiyo, huku wanajeshi wa Israel wakishambulia kwa mabomu madaraja na kuharibu nyumba katika shambulizi la kijeshi linaloongezeka.
Maoni ya Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich yalikuwa ya wazi zaidi kuliko yote yaliyotolewa na afisa mkuu wa Israeli kuhusu kukalia eneo la Lebanon katika mapigano ambayo Israeli inasema inawalenga wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran.
Lebanon iliingizwa kwenye vita vya kikanda mnamo Machi 2 wakati Hezbollah iliporusha makombora kuelekea Israeli.
Tangu wakati huo, Israel imewaamuru wakaazi wote kuhama kusini mwa Mto Litani huku ikifanya mashambulizi ya anga eneo hilo, kwa kuliona kama ngome ya Hezbollah, ambayo imekuwa ikiendeleza mashambulizi ya roketi dhidi ya Israel.
Maafisa wa Lebanon wanasema shambulizi la anga na ardhini la Israel limeua zaidi ya watu 1,000, na zaidi ya milioni moja wamefurushwa kutoka makazi makwao.
Mashahidi wa Reuters walisikia takriban milipuko mitatu katika wilaya ya Dahiyeh ya Beirut mwishoni mwa Jumatatu, huku jeshi la Israeli likisema kuwa lilikuwa limeshambulia maeneo ya Hezbollah katika mji huo.
Mashambulizi ya awali huko Beirut siku ya Jumatatu yalimuua kamanda wa Kikosi cha wasomi cha Quds cha jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, jeshi la Israel lilisema.
Soma zaidi:
Watu wakamatwa Nigeria baada ya video kusambaa mtandaoni za unyanyasaji wa kingono katika tamasha
Polisi nchini Nigeria wanasema watu 15 wamekamatwa kufuatia madai ya unyanyasaji wa kingono katika tamasha la jamii moja kusini mwa jimbo la Delta.
Video zilisambaa mtandaoni zikiwaonyesha vijana wakishambulia wanawake waliokuwa peke yao hadharani. Video hizo zilisababisha hasira kubwa, na kuwa chanzo cha hashtag #StopRapingWomen kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, na kuamsha wito wa uwajibikaji kuhusu ukatili wa kijinsia.
Polisi wa jimbo la Delta wamekanusha madai yanayosambaa mtandaoni kwamba tamasha la Alue-Do huko Ozoro lilikuwa "tamasha la ubakaji".
Msemaji wa eneo hilo Bright Edafe aliambia Channels TV siku ya Jumatatu alisema kwamba hakuna ripoti rasmi ya ubakaji iliyotolewa kuhusiana na tamasha hilo.
Video hizo, zilizopigwa wakati wa tamasha la uzazi la Alue-Do katika jiji la Ozoro, zinaonyesha makundi ya vijana wa kiume wakiwafukuza, wakiwavua nguo, wakiwakamata na kuwashambulia wanawake katika maeneo ya umma, katika baadhi ya matukio wakati watu wanarekodi
Msemaji wa polisi alielezea matukio hayo kama "ya kutisha, ya kuchukiza na ya aibu" na akasema wamewakamata washukiwa kadhaa waliotambuliwa kutoka kwenye video hizo na kuwahamisha kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai ya serikali (CID).
Edafe aliambia Channels: "Tumezungumza na wasichana wanne na wote walisema hakuna aliyewabaka."
Miongoni mwa waliokamatwa ni kiongozi wa jamii husika aliyetajwa sana kama mratibu wa tukio hilo.
Polisi wanasema uchunguzi unaendelea.
Pia unaweza kusoma:
Waziri wa zamani wa mambo ya nje Kenya akamatwa kwa kupanga kutoweka kwake
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje nchini Kenya, Raphael Tuju, amekamatwa siku moja baada ya kuripotiwa kutoweka, na kusababisha hofu kwamba huenda alitekwa nyara.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mohamed Amin alisema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Tuju alikuwa ndani ya nyumba yake wakati wote, akielezea tukio hilo kama "kutoweka kwa uangalifu badala ya kesi halisi ya utekaji nyara".
Kabla tu ya kukamatwa kwake, Tuju alikuwa ameambia kituo cha televisheni cha Citizen cha eneo hilo kwamba alikuwa amejificha baada ya kufuatwa na gari lisilo na usajili.
Waziri huyo wa zamani amekuwa akikabiliwa na kesi ya muda mrefu ya kisheria inayopinga mnada na umiliki wa mali zake jijini Nairobi unaotokana na mkopo wa benki ambao haujalipwa.
Amin alisema: "Mwenendo wa makusudi wa Raphael Tuju unaonekana kuwa uliopangwa kwa makusudi ya kudanganya umma ili kupata huruma isiyo na msingi na kudhoofisha uadilifu wa Huduma ya Polisi ya Kitaifa."
Aliongeza kuwa polisi wanachukulia "utoaji wa taarifa za uongo kwa mamlaka kama kosa kubwa sana".